• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:25 PM
DOUGLAS MUTUA: ‘Mashujaa’ wanaoibia umma wafungwe jela

DOUGLAS MUTUA: ‘Mashujaa’ wanaoibia umma wafungwe jela

Na DOUGLAS MUTUA

NI kauli yangu kwamba shujaa hafai kudai tuzo yoyote; hivyo, mashujaa waliopigania uhuru kote Afrika hawapaswi kutushinikiza tuwatuze ikiwa hatutaki.

Vilevile, nashikilia kuwa kila anayejinyakulia mali ya umma kwa kisingizio kwamba alipigania uhuru, anapaswa kuchukuliwa hatua kali bila huruma.

Yeyote aliyekuwa hai wakati ambapo mashujaa wa uhuru waliingia misituni kupambana na wakoloni, mradi hakuwasaliti, ni mashujaa pia.Hakuna kamanda asiye na jeshi, nalo jeshi haliwi jeshi pasipokuwa na wazalendo, wanaoliunga mkono na kulihimiza lihimili makombora huku nalo likirutupa yao.

Hii ina maana kwamba tukiamua kuwatuza mashujaa au kuwaruhusu wajitwalie kila wanachokitaka, kisa na maana walipigania uhuru, basi wapo kwa mamilioni.

Ipo siku itakayokucha walioiba walazimishwe kurejesha mali ya umma, lau sivyo wajipate korokoroni. Ikiwa una shaka na hili, uliza yanayoendelea Afrika Kusini wakati huu.

Labda historia ya hivi karibuni unayokumbuka kumhusu mfungwa maarufu zaidi Afrika Kusini wakati huu, Jacob Zuma, ni kwamba alitawala nchi hiyo kwa miaka tisa.

Miaka mingi tu kabla ya watu weusi kuondoa utawala wa wabaguzi wa rangi, Zuma alikuwa mkuu wa ujasusi wa chama cha African National Congress (ANC) kilicholeta ukombozi huo.

Kutokana na harakati zake hizo za kupigania uhuru, Zuma alifungwa miaka 10 kwenye gereza la Robben Island alikokuwa shujaa wa uhuru na rais wa kwanza mweusi, marehemu Nelson Mandela.

Kwa vyovyote vile, Zuma ni shujaa wa ukombozi wa watu weusi wanaoitawala Afrika kusini kwa sasa. Kwa hilo itabidi mnyonge umnyonge na haki yake umpe tu.

Hata hivyo, amerudi jela tena kwa utundu wake wa kudharau sheria na mahakama; kujitia hamnazo kabisa anapoitwa kueleza anayojua kuhusu ufisadi.

Sikwambii pia vitendo vya kula njama za kupora fedha za umma kwa viwango vya kusikitisha na kufedhehesha, wakati uo huo akishupaa shingo kana kwamba yeye ndiye sheria.

Ni sadfa iliyoje kwamba ameanza kutumikia kifungo cha miezi 15 juzi, wakati ambapo jirani yetu Sudan Kusini inapaswa kuwa ikisherehekea miaka 10 ya uhuru kutoka Sudan.

Rais Salva Kiir Mayardit amesema serikali yake haitaandaa sherehe zozote kutokana na matatizo ya kifedha na kisiasa nchini humo.

Aidha, ameilaumu sana jamii ya kimataifa kwa kuiwekea nchi yake vikwazo, ambavyo anaita adhabu, na hivyo kuiletea umaskini.Ukweli ambao Rais Kiir hawezi kukariri ni kwamba, huku nchi yake ikiendelea kudidimia kwenye lindi la umaskini, yeye na wakuu wengine serikalini wanaendelea kutajirika.

Wanaiba rasilimali za nchi na kuzificha Sudan, Kenya, Uganda, Ethiopia, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Djibouti na kwingineko.

Lakini wanapozungumzia matatizo ya taifa lao wanalia na kupiga mayowe kama waombolezaji wa kulipwa, ambao humlia marehemu kuliko waliopatwa na msiba huo.

Ukimsikia Rais Kiir anavyotupatupa maneno kiholela huku akimlaumu kila kiongozi wa upinzani na nchi anazoshuku ni adui, utajiuliza Sudan Kusini imedumishwa na nini kwa miaka 10.

Hana hulka ya kiongozi, ni mporaji nambari moja, na angali anashikilia kopo mkononi kuombaomba misaada kutoka nje huku akikalia madini na mafuta nchini mwake.

Ipo siku itakayokucha na Sudan Kusini ipate kiongozi asiyependa masihara, wezi wote wa sasa wajipate jela kama Zuma. Na hiyo itakuwa siku njema.

Mradi raia wa taifa hilo hawafurahii mambo yanavyokwenda, atazuka mmoja awajibishe kila fisadi. Na hiyo itakuwa siku njema.

[email protected]

You can share this post!

Museveni ataka nchi zote za Afrika zitumie Kiswahili

WANDERI KAMAU: Korti zetu ziige mataifa mengine kuboresha...