• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:55 AM
Hali tete miili ikianza kuzagaa Gaza huku Israel ikipanga mashambulio ya ardhini

Hali tete miili ikianza kuzagaa Gaza huku Israel ikipanga mashambulio ya ardhini

JERUSALEM, ISRAELI

NA MASHIRIKA

ISRAELI jana iliendelea kuushambulia vikali ukanda wa Gaza kwa makombora ya ndege, huku vikosi vyake vikijitayarisha kuanzisha mashambulio ya ardhini.

Hapo jana, Umoja wa Mataifa (UN) ulionya kuwa mashambulio hayo yamewafanya raia katika ukanda huo kukosa mahali mbadala pa kutafuta hifadhi.

Katika dalili zinazoonyesha vita hivyo vinaendelea kuenea, ndege moja ya Israeli pia ilitekeleza mashambulio kusini mwa Lebanon jana alfajiri, huku majeshi yake yakiendelea kukabiliana na Wapalestina katika eneo la West Bank.

Mnamo Jumapili, mashirika ya kutoa misaada yaliendelea kupeleka misaada zaidi kwa waathiriwa wa mapigano hayo Gaza.

Hata hivyo, mashirika ya kimisaada ya UN yalisema misaada iliyopelekwa katika eneo hilo ni sehemu tu ya misaada mingi inayohitajika kuwasaidia maelfu ya waathiriwa wa vita hivyo.

Kulingana na UN, waathiriwa wanahitaji misaada ya chakula, maji, dawa na mafuta.

Jana, vikosi vya afya eneo la Gaza vilisema kuwa karibu watu 4,600 wamefariki kutokana na mashambulio ambayo yamekuwa yakitekelezwa na Israeli kwa muda wa majuma mawili kufikia sasa. Hilo linafuatia shambulio lililotekelezwa na Hamas dhidi ya raia wake mnamo Oktoba 7, ambapo watu 1,400 waliuawa huku wengine 212 wakitekwa nyara.

Jana asubuhi, jeshi la Israeli lilisema kuwa kwa saa 24 zilizopita, lilifanikiwa kuyashambulia zaidi ya maeneo 320 Gaza, yanayoaminika kuwa ngome na maficho ya wapiganaji wa Hamas. Maeneo yaliyoshambuliwa yanajumuisha mtaro mmoja mkubwa unaotumika kama hifadhi ya wanamgambo hao.

Kwenye taarifa, jeshi hilo lilisema “liliyashambulia maeneo yanayohatarisha usalama wa wanajeshi wake wanaojitayarisha kwa mashambulio ya ardhini dhidi ya Gaza.”

Vyombo vya habari vya Palestina viliripoti kuwa mashambulio ya Israeli yalilenga maeneo ya kaskazini na kati ya ukanda wa Gaza.
Kulingana na vyombo hivyo, shambulio moja karibu na kambi ya wakimbizi ya Jabalia, kaskazini mwa Gaza, liliwaua Wapalestina kadhaa na kuwajeruhi wengine.

Kwa sasa, majeshi na vifaru vya Israeli wamepiga kambi katika mpaka wa taifa hilo na Gaza, ikielezwa wanangoja kuanza operesheni kali dhidi ya Hamas.

Hata hivyo, haijabainika ni lini vikosi hivyo vitaanza mashambulio ya ardhini.

Naibu balozi wa Israeli nchini Amerika, Eliav Benjamin, alisema kuwa kuna dalili Amerika imelirai taifa hilo kungoja zaidi kabla ya kuanza mashambulio ya ardhini.

“Israeli na Amerika zimekuwa kwenye mazungumzo tangu mzozo huu ulipoanza. Tunafuatilia kwa kina kuona hali itakavyokuwa kabla ya kuanza mashambulio ya ardhini,” akasema.

Mashambulio ya angani yamesababisha uharibifu mkubwa wa majengo katika eneo la Gaza.

Watu 1.4 milioni wakakisiwa kuathiriwa na mashambulio hayo kati ya wakazi 2.3 milioni wanaoishi ukanda huo.

  • Tags

You can share this post!

Slayqueen aachwa kwa mataa sponsa aliporudi kwa mkewe

Maskini Raila! Viongozi watoa sababu za kumhepa

T L