• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 4:43 PM
Maskini Raila! Viongozi watoa sababu za kumhepa

Maskini Raila! Viongozi watoa sababu za kumhepa

NA RUSHDIE OUDIA

WANASIASA ambao wamemwasi na kumtoroka kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, wamejitokeza na kueleza sababu zilizosababisha wao kumtoroka kigogo huyo wa kisiasa.

Bw Raila amejipata pabaya kisiasa katika siku za hivi karibuni, huku wanasiasa wengi waliokuwa wandani wake katika ngome yake ya Nyanza, wakimwasi na kuanza kushirikiana na Rais William Ruto na serikali yake ya Kenya Kwanza.

Wanasiasa hao walieleza mahangaiko na mateso waliyopitia katika ODM kabla ya kuamua kumwasi Bw Raila.

Wanataja udikteta, ‘utumwa’, ghasia, hadaa na kuaibishwa hadharani miongoni mwa mateso mengine kama kiini hasa cha kumkimbia kinara wao.

Rais Ruto amekuwa akiendesha mikakati ya kujizolea ufuasi wa kisiasa katika ngome za Bw Raila kwa kuwashawishi wanasiasa hao kujiunga na mrengo tawala.

Baadhi ya wanasiasa ambao wamemwasi Bw Raila na kujiunga Kenya Kwanza ni aliyekuwa msemaji wa Idara ya Kitaifa ya Polisi Charles Owino, wabunge wa zamani Ayiecho Olweny (Muhoroni), Elizabeth Ongoro (Kasarani), Bw Joe Donde (Gem), Edick Anyanga (Nyatike), Joshua Nyamori (mwanaharakati), Bw Odoyo Owidi, na kiongozi wa zamani wa vijana katika ODM na aliyekuwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Kisumu Samuel Ong’ow.

Wanasiasa wengine ambao wameamua kushirikiana na Dkt Ruto ni Seneta wa Kisumu Tom Ojienda, wabunge Mark Nyamita (Uriri), Elisha Odhiambo (Gem), Dkt Gideon Ochanda (Bondo), Paul Abuor (Rongo), Phelix Odiwuor almaarufu ‘Jalang’o’ (Langata) na Caroli Omondi (Suba Kusini).

Baadhi ya wanasiasa kama aliyekuwa Gavana wa Kisumu, Bw Jack Ranguma wamepata uteuzi serikalini kwa kumwacha Bw Raila. Mnamo Jumapili, Bw Olweny alikuwa mwanasiasa wa hivi majuzi zaidi kuasi Bw Raila. Alipokelewa na “mjumbe” mkuu wa Dkt Ruto, Waziri wa ICT, Eliud Owalo, nyumbani kwake Asembo, Siaya.

Prof Olweny aliwaeleza wananchi kuhusu mahangaiko aliyopitia katika ODM alipofurushwa nje ya ofisi Oktoba 19, 2022, katika mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Ofafa Memorial, Nairobi kwa madai kuwa hakuwa amealikwa.

“Hiyo ndiyo siku nilibaki bila chama. Nimekuwa huru tangu wakati huo. Kabla ya tukio hilo, nilikuwa nimepakwa tope na kuhangaishwa mara nyingi hadharani kabla ya hatimaye kufurushwa kutoka ODM,” akasema Prof Olweny.

Akionekana kumshambulia Bw Raila, mbunge huyo wa zamani alisema, “Lazima tukubali kuwa mtu mwingine anaweza kuiongoza nchi hii wala si mtu mmoja kila wakati. Tulikuwa na nguvu na ufuasi mkubwa ingawa lazima tukubali kuwa tulishindwa. Sioni yeyote akimshinda (Rais Ruto) kwenye uchaguzi ujao.”

Mwanasiasa huyo alisema alijiunga na kundi lililokuwa likimuunga mkono Bw Raila kama kijana mnamo 1992, mara tu baada ya kumaliza shahada yake ya uzamifu (PhD).

Sawa na Prof Olweny, Bi Ongoro, aliyehudumu kama Seneta Maalum na mbunge wa Kasarani, alisema walikuwa katika ODM kwa muda mrefu, kiasi cha kuamini kuwa hakuna chama kingine ambacho kingeikomboa kisiasa jamii ya Waluo kama si chao.

“Kama jamii, tumekuwa kwenye utumwa wa kisiasa kwa muda mrefu sana hadi tukasahau uhuru ambao tumekuwa nao. Lazima tukubali kwamba wakati mwafaka wa jamii hii kukombolewa umewadia. Hiyo ndiyo sababu imenifanya kuwa katika UDA kwa hiari,” akasema Bi Ongoro.

Bi Ongoro alisema jamii hiyo imekuwa katika mstari wa mbele kupigania uwepo wa vyama vingi vya kisiasa, hivyo haipaswi kumzuia kiongozi yeyoye kufurahia uhuru wake kulingana na Katiba.

Bw Owidi alirejelea jinsi walivyokuwa wakiteseka katika ODM.

“ODM ni chama kilichojaa hadaa ya kisiasa. Hakukuwa na ushindani wowote. Ni wakati mzuri wa mtindo wa ghasia na kutovumiliana kukoma,” akasema.

Kuhusu Bw Owino, tatizo kuu katika ODM limekuwa ni ghasia za kisiasa.

Alisema maendeleo yaliyopelekwa na Rais Ruto si ya kuwashawishi kujiunga na UDA, bali ni kwa manufaa ya wenyeji na eneo zima la Nyanza.

Hata hivyo, aliyekuwa spika wa bunge la Kaunti ya Kisumu, Bw Onyango Oloo, anawalaumu baadhi ya ‘waasi’ hao akisema baadhi yao ndio wamekuwa wakichochea fujo na ghasia ndani ya ODM.

Bw Oloo anadai kuwa chini ya Prof Olweny, ODM ilishuhudia ufisadi wa juu zaidi Kisumu, ubarakala na utawala wa kiimla usiokuwa na mfano.

“Bw Raila alimfanya kuwa mbunge na waziri msaidizi, ishara tosha kuwa chama cha ODM kilikuwa makazi mazuri zaidi. Hakuwa na msimamo wala sera, maono au dira. Mungu msaidie katika safari yake mpya,” akasema Bw Oloo.

  • Tags

You can share this post!

Hali tete miili ikianza kuzagaa Gaza huku Israel ikipanga...

SHINA LA UHAI: Teknolojia mpya ya CyberKnife tumaini la...

T L