• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Hamas yaachilia mateka wawili wakongwe wa Israel misaada ikianza kumiminika Gaza

Hamas yaachilia mateka wawili wakongwe wa Israel misaada ikianza kumiminika Gaza

NA XINHUA

JERUSALEM, ISRAELI

WANAWAKE wawili wakongwe waliotekwa nyara na Hamas waliachiliwa jana huku Israeli ikiimarisha mashambulizi ya anga yanayolenga Gaza.

Katika taarifa, Hamas, ilisema iliwaachilia wawili hao kwa kuwa wanahitaji misaada ya kibinadamu kutokana na umri wao.

Kituo cha habari cha televisheni cha Kan kinachomilikiwa na serikali ya Israeli kilitangaza kuwa wawili hao ni Yocheved Lifshitz, 85, na Nurit Cooper, 79.

Mume wa Yocheved, Oded Lifshitz, mwandishi wa habari mwenye umri wa miaka 83, alitekwa nyara na mkewe na bado anazuiliwa na Hamas.

Hii ni mara ya pili kwa Hamas kuwaachia huru baadhi ya waliotekwa nyara.

Afisa wa serikali ya Israeli alithibitisha kuachiliwa kwa Waisraeli hao wawili waliofika kwenye kivuko cha Rafah kati ya Gaza na Misri, na kuongeza kuwa timu ya Israeli ilikuwa njiani kuwachukua.

Mapema Jumatatu, duru za Palestina zilisema kuwa Hamas inapanga kuwaachilia wengine wa kigeni waliokamatwa huko Gaza kufuatia juhudi kali za upatanishi zilizofanywa na Qatar, Misri na Umoja wa Mataifa.

Imebainika pia kwamba idadi ya waliotekwa huko Gaza sasa inafikia 222, akiongeza kuwa ni pamoja na Waisraeli, raia wa kigeni, wanawake, watoto na wazee.

Haya yanajiri wakati shehena ya tatu ya misaada ya kibinadamu ikifika katika eneo la pwani kupitia kivuko cha Rafah.

Shirika la Palestinian Red Crescent lilithibitisha kwamba limepokea msafara wa tatu wa lori 20 zilizobeba misaada ya kibinadamu yenye chakula, maji, dawa na vifaa vya matibabu.

Wakati huo huo, ndege kutoka Algeria, Kuwait, Iraq, Türkiye, Falme za Kiarabu, na Shirika la Afya Duniani zilizobeba misaada ya kibinadamu kwa Ukanda wa Gaza ziliwasili katika Uwanja wa ndege wa al-Arish nchini Misri, ambao uko kilomita 50 kutoka kivuko cha Rafah.

Waziri wa Afya wa Uturuki Fahrettin Koca, alisema siku ya Jumatatu kuwa Türkiye ilituma ndege mbili za mizigo nchini Misri zikiwa zimebeba vifaa vya matibabu na vifaa vingine, na kuongeza kuwa ndege mbili zaidi zitatumwa na vifaa zaidi.

Hata hivyo, idadi ya walioangamia kwenye mapigano hayo yanaendelea kupanda.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina yenye makao yake makuu Ukanda wa Gaza, Wapalestina wasiopungua 436 waliuawa katika muda wa saa 24 zilizopita, na kufanya jumla ya vifo vya Gaza kufikia angalau 5,087, ambayo inajumuisha karibu watoto 2,055.

Mzozo huo pia umeua zaidi ya watu 1,400 nchini Israeli.

Jeshi la Israeli liliripoti kuuawa kwa makamanda watano wa jeshi la anga la Hamas, wanaohusika na ulinzi wa anga wa Gaza, pamoja na wanamgambo 12.

  • Tags

You can share this post!

Esther Musila afurahia tuzo ya kufanya kazi UN kwa muda...

Spika wa Seneti akataa wazo la chama chake cha PAA kumezwa...

T L