• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Harmonize motoni Nairobi kwa kukosa kuimba vilabuni

Harmonize motoni Nairobi kwa kukosa kuimba vilabuni

NA MERCY SIMIYU

MWANAMUZIKI Rajab Abdul Kahali, maarufu kama ‘Harmonize’ kutoka Tanzania, Jumapili jioni aliachiliwa na polisi baada ya kukamatwa asubuhi kwa madai ya kutofika katika vilabu kadhaa jijini Nairobi kutumbuiza licha ya kulipwa.

Mwanamuziki huyo alipangiwa kutumbuiza katika vilabu vya Volume001, Captain’s Lounge eneo la Athi River na Cocorico kilichoko Roysambu.

Lakini kwenye kikao na wanahabari katika Kituo cha Polisi cha Kileleshwa, mwanamuziki huyo alisema kuwa kulingana na mkataba wa kandarasi yake, alipaswa kukutana na mashabiki wala si kuwatumbuiza.

Alisema kulikuwa na hali ya kutoelewana baina ya mawakala wake na wenye vilabu hivyo.

Kulingana na Joe Barsil, ambaye ni mkurugenzi wa Captain’s Lounge, mwanamuziki huyo, ambaye pia anajiita Konde Boy, aliwatumbuiza mashabiki kwa muda wa dakika tano pekee.

“Nililipa Sh450,000 kwa kampuni ya Melamani Limited ili Harmonize kuja na kutumbuiza kwa muda wa saa moja na nusu. Hata hivyo, aliwatumbuizia mashabiki kwa dakika tano pekee,” akasema mkurugenzi huyo.

DJ Kay254ke wa Cocorico Club alisema walikuwa wamelipa Sh300,000 lakini Harmonize hakutokea.

Volume001 nao waliripotiwa kulipa Sh350,000.

Baadaye aliondoka polisi akiandamana na aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko akisema angetumbuiza jijini Mombasa, Jumapili usiku.

Harmonize aliomba radhi kwa kile alischosema ni hali ya kutoelewana iliyoibuka kati ya wenye vilabu husika na kampuni iliyokuwa ikiandaa burudani yake.

  • Tags

You can share this post!

Raila arai wakazi wa Mlima Kenya kwa kuahidi kuimarisha...

Aliyejaza nafasi ya Usain Bolt ajitosa Kip Keino Classic

T L