• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Aliyejaza nafasi ya Usain Bolt ajitosa Kip Keino Classic

Aliyejaza nafasi ya Usain Bolt ajitosa Kip Keino Classic

GEOFFREY ANENE na AYUMBA AYODI

BINGWA wa Olimpiki mbio za mita 100, Marcell Jacobs, ni mmoja wa mastaa wa kigeni wanaotarajiwa jijini Nairobi juma hili, kunogesha riadha za kimataifa za Absa Kip Keino Classic uwanjani Kasarani mnamo Mei 7.

Mwitaliano huyo atashiriki mbio za mita 100.

Atakutana na mshikilizi wa rekodi ya Afrika Ferdinand Omanyala na Waamerika matata Fred Kerley, Mike Rodgers na Isiah Young, miongoni mwa wengine.

“Mei 7. 100m. Nairobi Kenya. Twende kazi!” aliandika Jacobs kwenye Twitter.

Mkurugenzi wa mashindano ya Kip Keino Classic, Barnaba Korir, alisema kuwa Jacobs aliingia makala hayo ya tatu Jumamosi usiku.

Bingwa huyo wa Olimpiki pia alishinda taji la 60m majuzi wakati wa Riadha za Dunia za Ukumbini nchini Serbia mwezi Februari.

Mzawa wa Amerika, Jacobs ameinuka kujaza nafasi ya raia wa Jamaica, Usain Bolt, kama mtimkaji mwenye kasi ya juu kabisa duniani.

“Tunajivunia sana kuvutia majina makubwa sio tu katika 100m, bali pia katika vitengo vingine. Hiyo ndio sababu tunataka Wakenya wajitokeze kwa wingi kushuhudia wanariadha wetu wakikabiliana na magwiji wa dunia,” akasema Korir.

Kitengo cha akina dada cha mbio fupi pia kimevutia bingwa wa dunia 100m, Shelly-Ann Fraser-Pryce kutoka Jamaica, na Mwamerika Sha’Carri Richardson.

Pia, kuna bingwa wa Kip Keino Classic mbio za 200m, Christine Mboma, na mwenzake pia kutoka Namibia Beatrice Masilingi, aliyenyakua medali za fedha katika 100m na 200m kwenye Riadha za Dunia za U20 jijini Nairobi mwaka 2021.

Malkia wa Olimpiki 3,000m kuruka viunzi na maji Peruth Chemutai kutoka Uganda pia atashiriki.

Mfalme mara nne wa dunia katika kurusha kitufe Pawel Fajdek na malkia wa Olimpiki kwenye fani hiyo Anita Wlodarczyk, wote kutoka Poland pia watatua Nairobi.

Riadha hizo zitapeperushwa na runinga ya NTV. Tuzo ya washindi wa vitengo vya kimataifa ni Sh579,000 na vitengo vya Wakenya ni Sh50,000.

  • Tags

You can share this post!

Harmonize motoni Nairobi kwa kukosa kuimba vilabuni

WANDERI KAMAU: ‘Deni’ ametuacha nalo Kibaki kwa...

T L