• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Israel yaua 47 katika kambi ya wakimbizi Gaza ikiandama kamanda wa Hamas

Israel yaua 47 katika kambi ya wakimbizi Gaza ikiandama kamanda wa Hamas

Na AFP

UKANDA WA GAZA, Palestina

WATU 47 wameuawa baada ya wanajeshi wa Israeli kushambulia kambi kubwa ya wakimbizi katika Ukanda wa Gaza.

Israeli ilisema miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo la Jumanne jioni, ni kamanda mmoja wa kundi la Hamas aliyehusika katika shambulio la Oktoba 7 dhidi ya taifa hilo la kiyahudi.

Shambulio la Jumanne liliharibu majengo na kuacha mashimo makubwa yaliyojaa vifusi katika kambi hiyo ya Jabalia yenye idadi kubwa ya watu.

Milio ilisikika kila mahali huku mamia ya watu wakichakura kwenye vifusi vya majengo wakisaka manusura.

Wanahabari wa shirika la AFP walishuhudia angalau maiti 47 zikitolewa kutoka kwa vifusi hivyo.

Mkazi Ragheb Aqal, 41, aliyejawa na woga alifananisha mlipuko huo na “tetemeko la ardhi” kwani nyumba zilianguka na watu wengi kuzikwa kwenye vifusi.

Israeli ilisema ndege zake za kivita zilishambulia handaki kubwa katika kambi hiyo na “kuua idadi kubwa ya magaidi wa Hamas, akiwemo mmoja wa makamanda wao, Ibrahim Biari.

Msemaji wa Jeshi Johathan Conricus, alimtaja Biari kama “nguzo kuu katika upangaji na utekelezaji” wa mashambulio ya Hamas nchini Israel mwezi jana na kuua watu 1,400, wengi wao watoto.

Viongozi wa Israeli wameapa “kuponda kabisa” Hamas kama njia ya kulipiza kisasi shambulio baya zaidi kuwahi kutekelezwa na wapiganaji wa kundi hilo nchini humo.

Lakini shambulio la Jumanne jioni huenda likaongeza hasira kuhusu namna Israeli inavyoendesha vita hivyo na hasara yake kwa raia wa Palestina.

Wizara ya Afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas, ilishutumu tukio hilo na kulitaja kama mauaji ya kikatili yanayotekelezwa na Israeli.

Ilisema huenda idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Jabalia, ikapanda.

Wizara hiyo inadai kuwa ndani ya zaidi ya wiki tatu, mashambulio ya Israeli yamesabisha vifo vya zaidi ya watu 8,500 katika ukanda wa Gaza, thuluthi mbili kati yao, wakiwa wanawake na watoto.

Awali, Bolivia ilisema kuwa itakatiza uhusiano wa kidiplomasia na Israeli kama njia ya “kulaani” shambulio la Israeli eneo la Gaza.

Aidha, Qatar imeonya kuwa mashambulio yanayoendelezwa na Israeli huenda yakahujumu juhudi za kuhimiza kukomeshwa kwa vita na kufanyika kwa mazungumzo ya upatanisho.

Maafisa kadha wakuu wa Hamas wanaishi Qatar ambayo inaendeleza juhudi za kuhimiza kuachiliwa kwa mateka 240 wanaoaminika kutekwa na wapiganaji wa Palestina mnamo Oktoba 7.

Saudi Arabia pia ilishutumu shambulio hilo, ikisema ni kinyume cha haki za kibinadamu kwa “wanajeshi wa Israeli kushambulia kambi ya wakimbizi ya Jabalia.”

Lakini hukuna dalili kwamba mapigano hayo yatatulia.

Mashambulio ya angani yakiendelea, Israeli, jana ilisema wanajeshi wake saba waliuawa katika makabiliano na wapiganaji wa Hamas ndani ya Ukanda wa Gaza.

Kikosi cha Hamas kwa jina Ezzedine al- Qassam Brigades, kimeapa kugeuza Gaza kuwa “makaburi” ya wanajeshi wa Israeli.

  • Tags

You can share this post!

Bado tunapekua faili za Ezekiel, yasema afisi ya ODPP...

Jibaba lalia kilabuni baada ya vipusa kulinyima burudani

T L