• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mkongwe Roy Hodgson kuendelea kudhibiti mikoba ya Crystal Palace msimu wa 2023-24

Mkongwe Roy Hodgson kuendelea kudhibiti mikoba ya Crystal Palace msimu wa 2023-24

Na MASHIRIKA

ROY Hodgson amekubali kusalia kuwa kocha wa Crystal Palace msimu ujao wa 2023-24.

Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 75 anatarajiwa kutia saini mkataba mpya ugani Selhurst Park atakaporejea kutoka likizoni.

Hodgson alirejea ugani Selhurst Park kudhibiti mikoba ya Palace mnamo Machi 2023 baada ya kuaminiwa fursa ya kujaza pengo la Patrick Vieira aliyepigwa kalamu.

Alisaidia kikosi hicho kukwepa shoka la kuwateremsha daraja kutoka Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya Palace kujizolea alama 18 kutokana na michuano 10 iliyosimamiwa na Hodgson. Palace waliambulia nafasi ya 11 kwenye msimamo wa jedwali la EPL mnamo 2022-23.

Hodgson alihudumu kambini mwa Palace kwa miaka minne kuanzia 2017 ila akaamua kujiondoa kwenye ulingo wa ukocha mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Mkufunzi huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza aliteuliwa kuwa kocha wa Watford mnamo Januari 2022 ila akabanduka miezi mitano baadaye kikosi hicho kilipoteremshwa ngazi kutoka EPL hadi Ligi ya Daraja ya Kwanza (Championship).

Palace walikuwa wamepiga mechi 12 mfululizo bila kushinda chini ya Vieira hadi Hodgson aliporejea kambini mwa kikosi hicho.

Anajivunia tajriba pevu ya ukufunzi kwa zaidi ya miaka 45 iliyopita na amewahi pia kudhibiti mikoba ya Inter Milan, Blackburn, Fulham, Liverpool, West Brom na Palace. Hodgson amewahi pia kunoa timu za taifa za Uswisi, United Arab Emirates (UAE) na Finland.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Jinsi mamluki wa Wagner walivyosababisha kiwewe

Kenya Kwanza waita Azimio kwa majadiliano kuhusu uteuzi wa...

T L