• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Kindiki aonya Azimio kuhusu maandamano ya kupinga nyongeza ya VAT  

Kindiki aonya Azimio kuhusu maandamano ya kupinga nyongeza ya VAT  

Na MWANGI MUIRURI

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki Jumapili, Juni 18, 2023 aliapa kukabiliana na mrengo wa upinzani iwapo utaandaa maandamano kupinga kupitishwa kwa mswada wa Kifedha wa 2023.

Mswada huo unapendekeza nyongeza na pia shuka za ushuru (VAT), ukiwa na upinzani mkali miongoni mwa raia na pia mrengo wa upinzani unaoongozwa na Bw Raila Odinga.

Bw Kindiki alisema kwamba “ukishindwa katika mijadala, kura na vyovyote vile tena, usiwe wa kutusukumia vitisho vya maandamano ya fujo”.

Alikuwa akiongea katika kanisa la PEFA lililoko katika mtaa wa Kamahuha, Kaunti ya Murang’a.

Alisema kwamba Mswada wa Fedha 2023 utapita bungeni “na ikiwa hutaridhika una mwanya tu wa kwenda mahakamani ili kusaka afueni”.

Bw Kindiki alisema kuwa “Katiba inakubalia maandamano ya amani lakini yale ambayo tumekuwa tukisukumiwa hapa nchini ni ya kihuni, kijambazi na ya kutatiza maisha na uchumi”.

Akaongeza: “Ukiwaona hao wa maandamano uwaambie sisi hatutawavumilia kamwe…Wakithubutu tutawazima hata kabla wazindue maandamano hayo”.

Kanisa la PEFA la Kamahuha eneobunge la Maragua ambapo Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki mnamo Jumapili, Juni 18, 2023 aliapa kukabiliana na mrengo wa upinzani iwapo utaandaa maandamano kuhusu Mswada wa Kifedha 2023. Picha|MWANGI MUIRURI

Prof Kindiki alitumana “Ukimuona mfikishie ujumbe wangu kwamba hatumuogopi na hatutampa nafasi ya kuhujumu amani jinsi alivyofanya Februari…”

Februari 2023, muungano wa Azimio uliandaa maandamano jijini Nairobi na katika miji ngome kuu kushinikiza serikali kushusha gharama ya maisha.

Azimio pia iliweka matakwa kadha wa kadha ili kusitisha maandmano yake.

Waziri Kindiki alisema “Sio tu hao wa mrengo wa upinzani nalenga…Hata wale walio katika mrengo huu wetu wa serikali ni lazima wazingatie mbinu za amani katika kusuluhisha mizozo”.

Alisema kwamba “kunao ambao ni wa chama cha rais wetu ambao katika Kaunti ya Kericho wanasakamwa kuhusu vurugu zilizokumba mashamba ya majani chai yaliyo eneo hilo”.

Magenge ya vijana yalivamia baadhi ya mashamba hayo na kuharibu mali yakiteta kuhusu dhuluma za ajira.

Prof Kindiki alisema kwamba “tumeagiza hao wote wanaoshukiwa kuhujumu amani katika mashamba hayo waandikishe taarifa na iwapo ushahidi wa kuwashtaki utapatikana, sharti wajibu mashtaka”.

Alisema kwamba “wale walio katika mrengo wa serikali ndio wanafaa kuchukua tahadhari zaidi kwa kuwa sisi lazima tuweke mfano bora zaidi katika huduma kwa taifa na yeyote wetu ambaye atathubutu kuhujumu amani anapaswa aelewe atachukuliwa kama anayehujumu serikali na pia Rais wetu”.

Alisema kuwa ndani ya wizara yak, kumejaa maafisa ambao watajituma kufa kupona kuhakikisha amani imedumu nchini.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mbunge afichua kanisa Nairobi waumini hushiriki ngono bila...

Ushuru: Raila ni moto wa karatasi, adai Ruto

T L