• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Ushuru: Raila ni moto wa karatasi, adai Ruto

Ushuru: Raila ni moto wa karatasi, adai Ruto

BENSON MATHEKA na LEONARD ONYANGO

RAIS William Ruto amewataka wabunge wa Azimio la Umoja waliounga mkono au kuhepa shughuli ya kupigia kura Mswada wa Fedha wa 2023, kupuuza vitisho vya viongozi wa muunngano huo wa Upinzani.

Rais Ruto aliyeonekana kuwapongeza wabunge wa Azimio waliounga mkono au kukosa kufika Bungeni mnamo Jumatano kupigia kura Mswada wa Fedha wa 2023, aliwataka wabunge wa Upinzani kufuata matakwa ya wapigakura na wala si maelekezo ya wakuu wa vyama vyao.

Kwa mujibu wa Rais Ruto, Mswada huo umesheheni mapendekezo tele yanayolenga kuboresha uchumi na kuinua maisha ya walalahoi, almaarufu mahasla.

“Acheni maneno mengi, eti sijui umeandikiwa barua na chama gani. Wewe unayeandikiwa barua na chama, hawa ambao walikupigia kura umeisoma barua yao? Hawa ambao wanataka kazi, barua yao umesoma? Soma barua ya watu waliokuajiri,” akasema Rais Ruto alipokuwa akizungumza katika kanisa la Christ Church Cathedral, Kaunti ya Kakamega.

Wabunge wanatarajiwa kupigia kura Mswada wa Fedha 2023 kwa mara ya mwisho kesho. Rais Ruto alionekana kurejelea kinara wa ODM, Bw Raila Odinga ambaye ametishia kuwaadhibu wabunge wanne waliounga mkono mswada huo na wengine 24 waliokosa kufika Bungeni Jumatano, wiki iliyopita.

“Kwa mujibu wa kanuni za nidhamu za chama, ilani za kuwataka kueleza sababu kwa nini wasiadhibiwe, zimetumiwa wabunge hao. Wanatarajiwa kujibu ndani ya saa 48 zijazo,” Katibu Mkuu wa ODM, Seneta Edwin Sifuna.

Kulingana na Seneta Sifuna, chama hicho kilichukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamishi kuhusu hatua ya wabunge hao ya kukaidi maagizo ya vinara wa Azimio waliowataka kukataa mswada huo.

Wabunge wanne waliounga mswada huo ni Mwakilishi wa Kike wa Nairobi, Bi Esther Passaris, Aden Adow Mohamed (Wajir Kusini), Elisha Ochieng Odhiambo (Gem) na Caroli Omondi (Suba Kusini).

Miongoni mwa wabunge wa ODM waliokosa kufika Bungeni ni John Mbadi (Maalum), Gideon Ochanda (Bondo), Eve Obara (Kasipul), Babu Owino (Embakasi Mashariki) na Otiende Amollo (Rarieda).

Rais Ruto alipokuwa katika eneobunge la Githunguri, Kaunti ya Kiambu mnamo Jumamosi aliupigia debe mswada huo akisema kuwa unaungwa mkono na wabunge kadhaa wa Azimio la Umoja.

“Kama watu wa Upinzani waliunga mkono Mswada wa Fedha, mbona nyinyi mpinge?” akasema Rais Ruto huku akionekana kumshambulia mbunge wa Githunguri, Bi Gathoni wa Mucomba ambaye amepinga vikali mswada huo licha ya kuwa ndani ya Kenya Kwanza.

Jana, Rais Ruto alisema wabunge wanapaswa kuwajibika kwa wapigakura na kutaja wanaopinga ajenda ya serikali yake ya kutoza raia ushuru zaidi kama “watu wasiojali raia”.

Akitetea mswada huo, Rais alisema njia ya pekee ya kufanya Kenya kustawi ni kufadhili miradi kupitia ushuru badala ya “kubebesha raia mzigo wa madeni”.

Alihimiza wabunge kupitisha mswada huo akisema una mengi ya kufaidi Wakenya hasa vijana wasio na ajira kwa kulinda viwanda vya humu nchini.

“Kuna njia mbili za kufanya nchi kuendelea au kurudi nyuma. Njia ya kwanza ni ile ambayo Kibaki (Rais wa tatu wa Kenya) alitumia alipochukua uongozi. Alichukua usukani uchumi ukiwa wa Sh200 bilioni pekee, akaweka mipango ya kulipa madeni na alipoondoka uongozini aliacha ukiwa wa thamani ya Sh900 bilioni, karibu Sh1 trilioni, hiyo ni njia moja. Tukusanye ushuru,” alisema Rais.

Alisema njia ya pili ni ile aliyotumia mtangulizi wake Uhuru Kenyatta ya kukopa hadi akaacha nchi ikilemewa na mzigo wa madeni.

“Njia ya pili ni hii ya watu wa handisheki. Walichukua uongozi deni letu likiwa Sh4 trilioni, saa hii limefika Sh9 trilioni, karibu Kenya inapigwa mnada. Nyinyi mnataka tuendelee na hii ya mnada ama ya Kibaki ya kukusanya ushuru, kila mtu alipe,” alisema.

Mswada wa Fedha wa 2023 umekumbwa na upinzani mkali kwani unapendekeza kuongezwa kwa ushuru wa mafuta kutoka asilimia 8 hadi 16 – hatua ambayo itaongeza bei za bidhaa muhimu kama vile vyakula.

Wafanyakazi watakatwa asilimia 1.5 ya mishahara yao kufadhili mradi wa nyumba nafuu na sukari kutoka nje itatozwa ushuru wa Sh5 kwa kila kilo endapo mswada huo utapitishwa.

 

  • Tags

You can share this post!

Kindiki aonya Azimio kuhusu maandamano ya kupinga nyongeza...

Wabunge kutathmini pendekezo la ‘kugatua’ Kenya...

T L