• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Maafisa walaumiwa kwa kupendelea watu wa Trump

Maafisa walaumiwa kwa kupendelea watu wa Trump

Na MASHIRIKA

WASHINGTON D.C., Amerika

POLISI wamezidi kulaumiwa kwa kutotumia nguvu kuwakabili wafuasi wa Rais anayeondoka Donald Trump waliovamia majengo ya bunge.

Rais Mteule Joe Biden, aliwalaumu maafisa wa usalama akisema walitumia nguvu zaidi walipozima waandamanaji waliolalamikia mauaji ya raia weusi nchini humo mwaka 2020 kuliko wale waliovamia majengo ya bunge Jumatano.

“Kama yangekuwa maandamano ya Black Lives Matter, wangekabiliwa kwa njia tofauti sana na jinsi genge la wakora waliovamia Capitol lilivyofanyiwa,” Biden alisema kwenye hotuba aliyotoa akiwa katika mji wa nyumbani kwake wa Delaware.

“Sote tunajua hilo ni kweli na halikubaliki,” alisema Biden ambaye ataapishwa kuwa rais Januari 20 baada ya kushinda uchaguzi wa urais wa Novemba 2020 kwa kuungwa mkono na wapigakura wengi wenye asili ya Kiafrika.

Mnamo Jumatano, maelfu ya waandamanaji waliochochewa na hotuba ya Rais Trump walivamia majengo ya bunge, ambapo baadhi yao walivunja vizuizi na milango katika tukio lililoonyeshwa moja kwa moja kwenye runinga.

Ilikuwa mara ya kwanza kitendo kama hicho kufanyika katika historia ya bunge la Amerika.

Lakini maafisa wa polisi wanaosimamia usalama walikataa kutumia gesi ya kutoa machozi hadi wavamizi walipoingia ndani ya jengo hilo wakisaka ofisi bila wasiwasi.

Vyombo vya habari nchini Amerika viliripoti kuwa baadhi ya maafisa wa polisi waliwafungulia milango waandamanaji hao.

Hali ilikuwa tofauti kabisa na maandamano ya kulalamikia ubaguzi wa rangi katika jiji hilo mwaka 2020 ambapo polisi walitumia nguvu kuwatawanya waandamanaji. Maafisa wa kikosi maalumu cha National Guard waliotumiwa kuwatawanya waandamanaji hao hawakufika kuzima maandamano ya Jumatano licha ya washiriki kutangaza hadharani mipango yao siku kadhaa zilizotangulia.

Waamerika wengi, wakiongozwa na wanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi, wamelaumu maafisa waliosimamia usalama Jumatano kwa kuwa na upendeleo.

“Tulitumia msimu wote wa joto uliopita tukipigania haki kwa watu kama George Floyd na Breonna Taylor, na tukafyatuliwa risasi za mpira,” Patrisse Cullors, mmoja wa waanzilishi wa vuguvugu la Black Lives Matter aliambia shirika la habari la CNN.

Cullors alimsifu Biden kwa kukemea maafisa wa polisi kwa kuonyesha upendeleo wa wazi akisema kitendo cha maafisa hao si haki kwa nchi na ulimwengu kwa jumula.

Michelle Obama pia alisema kwamba kama wafuasi wa Trump wangekuwa weusi wangeshughulikiwa kwa ukatili zaidi.

“Maandamano ya Black Lives Matter yalikuwa ya amani sana ilhali tuliona waandamanaji wakitawanywa kwa nguvu,” Michelle aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

“Hali ilikuwa tofuati kwa wale waliokufuru kitovu cha serikali ya Amerika wiki hii walipotolewa nje sio kwa kufungwa pingu lakini wakiwa huru waendelee na shughuli zao,” aliongeza Michelle.

You can share this post!

Mary Wambui apata kazi nyingine serikalini

SPANISH CUP: Barcelona wapewa limbukeni Cornella...