• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 2:21 PM
Maasi dhidi ya Putin yachacha maelfu wakitoroka Urusi

Maasi dhidi ya Putin yachacha maelfu wakitoroka Urusi

NA MASHIRIKA

MOSCOW, URUSI

POLISI jana Jumatatu walikabiliana na waandamanaji katika eneo la Dagestan nchini Urusi, huku pingamizi dhidi ya agizo la Rais Vladimir Putin kuwasajilisha raia kwa nguvu katika jeshi zikiendelea kuongezeka.

Rais Putin analenga kuwasajili hadi watu 300,000 kujiunga na jeshi la taifa hilo linaloshiriki vita nchini Ukraine.

Hayo yanajiri huku maelfu ya raia kutoka Urusi wakiendelea kutorokea katika mataifa jirani.

Kulingana na takwimu ambazo zimetolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Wakimbizi (UNHCR), karibu watu 50,000 kutoka Urusi wametorokea nchini Georgia, huku 40,000 wakikimbilia Armenia.

Kulingana na shirika la kutetea haki za binadamu la OVD-Info, zaidi ya watu 100 walikamatwa katika jiji la Makhachkala.

Shirika hilo lilieleza kusikitishwa na ripoti kuhusu “mateso” wanayopitia watu wanaozuiliwa katika sehemu tofautu nchini humo.

Wakazi wengi katika eneo hilo ni Waislamu na ndilo limeshuhudia idadi kubwa zaidi ya vifo nchini Urusi tangu vita kati yake na Ukraine kuanza.

Kwa jumla zaidi ya watu 2,000 wamekamatwa tangu maandamano hayo yalipoanza kupinga agizo la Rais Putin.

Maandamano hayo yakiendelea katika karibu miji yote mikubwa nchini humo, zaidi ya watu 700 walikamatwa Jumamosi pekee.

Picha zilizowekwa mitandaoni zilionyesha waandamanaji na polisi wakikabiliana katika eneo hilo.

Kwenye video moja, mwanamume aliyekuwa amezuiliwa na polisi anampiga polisi huyo kwa kichwa, kabla ya polisi kuungana na kuanza kumpiga mwanamume huyo.

Video nyingine inaonyesha afisa wa usalama akitoroka kutoka kwa kundi la waandamanaji. Kundi hilo lilikuwa limejaribu kumkamata.

  • Tags

You can share this post!

Ebola: Uganda yaripoti maambukizi, vifo zaidi

Gachagua aibuka bingwa wa kuteleza

T L