• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
Ebola: Uganda yaripoti maambukizi, vifo zaidi

Ebola: Uganda yaripoti maambukizi, vifo zaidi

NA DAILY MONITOR

KAMPALA, UGANDA

WIZARA ya Afya nchini Uganda jana Jumatatu ilisema kuwa idadi ya vifo vilivyosababishwa na ugonjwa wa Ebola imefikia 21, huku visa vya maambukizi vikifikia 34.

Visa hivyo vimeongezeka kutoka 31, vilivyokuwa vimethibitishwa Jumamosi.

Takwimu hizo ni kulingana na taarifa iliyotolewa na msemaji wa wizara hiyo, Emmanuel Ainebyooba.

Alisema kuwa visa vyote vimethibitishwa kutokana na sampuli za waathiriwa zilipelekwa katika Kituo cha Kitaifa cha Kuchunguza Virusi Uganda (UVRI).

Wilaya ya Mubende ndilo eneo lililoathiriwa zaidi na maambukizi.

“Visa vilivyothibitishwa nje ya wilaya ya Mubende ni vitatu katika wilaya ya Kyegegwa na kimoja katika eneo la Kassanda,” akasema.

Msemaji huyo alisema kuwa kinyume na ripoti za awali, hakuna kisa chochote ambacho kimethibitishwa jijini Kampala.

Maafisa wakuu wa jiji hilo walisema kuwa ripoti kamili kuhusu chanzo cha kifo cha mtu aliyeshukiwa kufariki kutokana na maradhi hayo jijini humo itatolewa hivi karibuni.

Kufikia Jumatatu, wilaya zilizokuwa zimethibitisha uwepo wa maambukizi ni Kassanda, Kampala, Kisoro, Kakumiro, Mubende, Kyegegwa na Lyantonde.

Wizara ya Afya imewaomba raia kuchukua tahadhari na kuripoti visa vyovyote wanavyoshuku ni vya maradhi hayo.

Kulingana na wizara hiyo, maradhi hayo huwa yanasambazwa kupitia damu, kinyesi au majimaji ya mwili kutoka kwa mtu aliyeambukizwa.

Yanaweza pia kusambazwa kupitia vifaa vilivyoguswa na majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa.

Mtu pia anaweza kuambukizwa kwa kugusa damu, viungo au majimaji ya mnyama aliyeambukizwa kama vile popo.

Baadhi ya dalili za maradhi hayo ni joto jingi mwilini, uchovu, maumivu ya kifua, kuharisha, kutapika, kuvunja damu katika sehemu tofauti mwilini na macho kubadilika rangi.

Wizara ya afya ilieleza kuwa mtu huanza kuvunja damu baada ya kuzidiwa na maradhi hayo.

Wikendi, wizara ilieleza kutoridhishwa na juhudi zinazoendelezwa kubaini watu waliotangamana na wale walioambukizwa.

Akihutubia jopokazi la kitaifa la kukabiliana na maradhi hayo katika wilaya ya Mubende mnamo Jumapili, kiongozi wa jopokazi hilo, Luteni Kanali Henry Kyobe alisema kuwa wanawatafuta watu 213 wanaoshukiwa kutangamana na watu walioambukizwa.

“Kwa sasa, tunawatafuta watu 213. Kuwatafuta watu hao ndiko changamoto kuu inayotukabili. Kati ya watu hao, 118 ni wahudumu wa afya. Hivyo, ili kufaulu kwenye juhudi hizo, itatulazimu kuboresha ushirikiano wetu zaidi,” akasema.

Waziri wa afya nchini humo, Jane Ruth Aceng, aliagiza juhudi hizo kuimarishwa ili kudhibiti maambukizi ya maradhi hayo.

“Jambo muhimu litakalotusaidia kudhibiti maradhi hayo ni kutambua watu waliotangamana na wale waliothibitishwa kuambukizwa. Si lazima tungoje serikali kutoa fedha ili kufanikisha juhudi hizo. Fedha zitatumwa, japo si lazima tungoje hadi wakati huo,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Serikali iweke mikakati ya kulinda wakulima...

Maasi dhidi ya Putin yachacha maelfu wakitoroka Urusi

T L