• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Mamia wauawa mpakani mwa Ethiopia na Somalia

Mamia wauawa mpakani mwa Ethiopia na Somalia

Na MASHIRIKA

ADDIS ABABA, ETHIOPIA

ZAIDI ya watu 100 wameuawa kwenye mapigano yanayoendelea katika maeneo ya mpakani kati ya Ethiopia na Somalia, wamesema maafisa wa serikali ya Ethiopia.

Kulingana na taarifa za serikali, mapigano hayo yamekuwa yakiendelea katika eneo la Afar, Ethiopia na maeneo mengine ya karibu na mpaka wa Somalia.

Wengi kati ya waliouawa ni wenyeji, hasa wachungaji.

Naibu Kamishna wa Polisi wa eneo la Afar, Ahmed Humed, alisema mapigano hayo yalianza wikendi iliyopita, baada ya vikosi vya Somalia vinavyohudumu katika eneo hilo kuwashambulia wenyeji wa Ethiopia.

Mapigano hayo yanajiri huku Ethiopia ikiendelea kujitayarisha kwa uchaguzi mkuu hapo Juni.

Wadadisi wanasema kuzuka upya kwa mapigano katika eneo hilo kunaashiria changamoto za kiusalama zinazomkabili Waziri Mkuu Abiy Ahmed, ikizingatiwa taifa hilo linakabiliwa na mapigano mengine yanayoendelea katika eneo la Tigray.

Msemaji wa serikali ya Somalia katika eneo hilo, Ali Bedel, alisema watu 25 waliuawa mnamo Ijumaa.

Vikosi vya Somalia vinadaiwa kuwashambulia na kuwaua watu wengine Jumanne. Somalia inadai kumiliki eneo la Afar.

Haikubainika mara moja ikiwa watu hao 25 ni kati ya 100 waliuawa.

Wakati huo huo, Ahmed Kaloyte, ambaye ni miongoni mwa maafisa wanaosimamia eneo hilo, alisema kikosi maalum cha polisi cha Somalia kilishirikiana na wanamgambo kuvamia eneo liitwalo Haruka na “kuwaua zaidi ya wakazi 30 ambao ni wachungaji wa kuhamahama.”

Inadaiwa zaidi ya watu 50 walijeruhiwa kwenye shambulio hilo.

“Wenyeji waliwakabili wavamizi hao na kufanikiwa kuwakamata baadhi yao. Hali ya kawaida ilirejea kwa muda,” akasema.

Mataifa hayo yamekuwa yakilaumiana kuhusu kuchipuka kwa ghasia hizo.

Mzozo huo unazuka wakati Abiy anajaribu kudhibiti hali katika eneo la Tigray.

Awali, uchaguzi mkuu wa Ethiopia ulipangiwa kufanyika Agosti mwaka uliopita, lakini ukaahirishwa kutokana na mchipuko wa janga la virusi vya corona.

Uchaguzi unatajwa kuwa mtihani mkubwa kwa Abiy, kwenye juhudi za kujaribu kurejesha umoja na uthabiti wa kisiasa katika taifa hilo.

“Vikosi vya Somalia vilishambulia maeneo ya Haruk na Gewane kwa silaha kali kama bunduki na gruneti. Watoto na wanawake waliuawa walipokuwa usingizini,” akasema Ahmed.

Mnamo Oktoba mwaka uliopita, watu 27 waliuawa kwenye wimbi la mapigano kuhusu umiliki wa eneo hilo tata.

Serikali ya Abiy pia inaelekezewa shinikizo kueleza kuhusu ripoti za kuchipuka upya kwa mapigano kati ya jamii za Oromo na Amhara, ambazo ndizo kubwa zaidi nchini humo. Abiy, aliye kiongozi wa kwanza kutoka jamii ya Oromo, alichukua uongozi wa taifa hilo mnamo 2018 baada ya serikali kushuhudia maandamano makubwa dhidi yake kwa miaka kadhaa.

Hata hivyo, utawala wake umekumbwa na msururu wa mapigano ya kikabila na umwagikaji damu.

  • Tags

You can share this post!

‘Tutakupeza Prof Ken Walibora’

MAKALA MAALUM: Vijana 2 wanaotengeneza mafuta kutokana na...