• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Mbwembwe mfalme akichukua usukani

Mbwembwe mfalme akichukua usukani

WANDERI KAMAU NA MASHIRIKA

MFALME Charles III wa Uingereza na mkewe, Camilla, jana Jumamosi walitawazwa rasmi kama mfalme na malkia wa Uingereza katika Ukumbi wa Westminister Abbey, jijini London kwenye sherehe ya kihistoria.

Ni hatua inayoashiria mwanzo mpya katika utawala wa kifalme nchini Uingereza kwa Mfalme Charles, ambaye amesubiri kwa zaidi ya miaka 70 kuchukua usukani.

Hafla kama hiyo iliandaliwa nchini humo mnamo 1953, wakati wa kutawazwa kwa marehemu Malkia Elizabeth II, kufuatia kifo cha babake, Mfalme George IV, baada ya kuugua.

Wakati huo, Malkia Elizabeth alikuwa ziarani nchini Kenya katika Kaunti ya Nyeri, kwenye Mkahawa wa Treetops, pembeni mwa Msitu wa Mlima Kenya.
Mfalme Charles alitawazwa kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth II, aliyefariki Septemba 8, 2022 katika Kasri la Balmoral, Uingereza. Charles alitawazwa mbele ya Askofu Justin Welby wa Canterbury kwa mafuta matakatifu na kula kiapo cha wafalme. Baadaye, alivishwa Taji la Kifalme la St Edward’s kichwani mwake na kushangiliwa kwa pamoja na washiriki: “Mungu Mwokoe Mfalme!”

Mbele ya wageni 2,300 wakiwemo zaidi ya marais 100 kutoka nchi tofauti, Mfamle huyo aliapa kuzingatia utamaduni wa dini ya Kiprotestanti nchini humo na kuhifadhi haki za Kanisa la Uingereza (Church of England) kama ilivyo kwenye sheria za taifa hilo. Marais hao walijumuisha Rais William Ruto wa Kenya. Rais Joe Biden wa Amerika aliwakilishwa na mkewe, Jill Biden.

Maelfu ya watu walikusanyika karibu na jengo hilo kutazama msafara maalumu kutoka Kasri la Buckingham kuelekea Abbey.
Msafara huo ulijumuisha wanajeshi 7,000 na bendi 19 za kijeshi—idadi inayotajwa kuwa kubwa zadi tangu kutawazwa kwa Malkia Elizabeth II mnamo 1953.

Hafla hiyo, ambayo ilikijita pakubwa katika tamaduni za kanisa la Kianglikana, huwa na umuhimu mkubwa.

Ilihusisha Charles kutawazwa, kupewa mavazi maalum ya kifalme na hatimaye kuvishwa. Pia, alisisitiza kujitolea kutekeleza majukumu yake ya kidini na kifalme.

Wawakilishi wa Kanisa la England na familia ya kifalme walitangaza heshima yao kwake. Watu tofauti kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola pia walialikwa kutangaza hayo. Kinyume na Charles, Camilla alitawazwa katika hafla fupi kiasi.

Baada ya hafla hizo, familia hiyo ilirejea katika Kasri la Buckingham kwenye msafara wa kijeshi.

Kinyume na hafla za hapo awali, hafla ya jana Jumamosi ilibadilishwa kidogo ili kuwakilisha imani tofauti, tamaduni na jamii kutoka sehemu tofauti nchini humo.

Hafla yenyewe ilikuwa fupi ikilinganishwa na ile ya kumtawaza Malkia Elizabeth 1953.

Kando na hafla hiyo, sherehe nyingine zilifanyika katika mataifa ya Australia, Canada, New Zealanda na visiwa vya Guernsey, Jersey na Isle of Man, vinavyodhibitiwa na kutawaliwa na Uingereza.

Licha ya utawazo huo kukamilika Jumamosi, sherehe hizo zitaendelea nchini humo hadi kesho Jumatatu.

Kutakuwa na tamasha maalumu ya utawazo leo Jumapili katika Kasri la Windsor, ambako wawakilishi wa mashirika ya Charles na Camilla ya kuisaidia jamii watahudhuria. Raia wa kawaida pia wataruhusiwa kushiriki.

Mpango mwingine, unaoitwa The Big Help Out unaolenga kuwahamasisha watu kushiriki katika mikakati ya kuisaidia jamii utafanyika katika Windsor Castle kesho Jumatatu na utapeperushwa moja kwa moja kwenye runinga na kupitia mtandao.

Kutakuwa na nishani maalum za uapisho zitakazotolewa nchini Uingereza na Canada.

  • Tags

You can share this post!

MFALME CHARLES III AVIKWA TAJI: Marais waalikwa wafuatilia...

Ahadi hewa ya Raila kwa wafanyabiashara

T L