• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Pigo kwa Gicheru ICC ikikataa ombi lake

Pigo kwa Gicheru ICC ikikataa ombi lake

Na VALENTINE OBARA

WAKILI Paul Gicheru, amepata pigo katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) baada ya ombi lake la kutaka kubadilishiwa jaji kukataliwa.

Bw Gicheru ameshtakiwa kwa madai ya kushawishi mashahidi wajiondoe kwa kesi za ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 zilizowandama Naibu Rais William Ruto.

Alikuwa ameomba mahakama hiyo imwagize Jaji Miatta Maria Samba ajiondoe katika kesi yake akidai kuwa hatamtendea haki.

Kulingana naye, jaji huyo alikuwa amehusika katika uchunguzi wa kesi za awali zilizohusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 nchini, na hivyo basi maamuzi yake katika kesi ya sasa hayatakuwa ya haki.

“Jopo la majaji lilikaa Oktoba 19, kutathmini ombi hilo na kwa uamuzi mmoja, majaji wakalikataa. Maelezo kuhusu sababu za majaji kutoa uamuzi huu yatatolewa baadaye,” akasema Rais wa ICC, Jaji Piotr Hofma?ski katika taarifa fupi.

Jaji Samba alikuwa amejitetea kuwa wakati alipokuwa afisa wa mipango ya ICC Uganda kati ya Oktoba 2006 hadi Oktoba 2010, alihusika katika baadhi ya shughuli za ICC nchini Kenya ila hakuwa na idhini ya kushiriki katika masuala yoyote ya kiupelelezi wala ushauri.

Ombi la Bw Gicheru lilikuwa limepingwa pia na upande wa mashtaka uliosema halina msingi.

Naibu Kiongozi wa Mashtaka, Bw James Stewart, alitaka ombi hilo litupwe nje kwa vile lilibashiri ubaguzi wa jaji hata kabla kesi ianze, na pia ilithibitishwa kuwa Jaji Samba alikuwa afisa wa ngazi za chini alipohudumia masuala ya Uganda na Kenya na hivyo basi haingewezekana kuwa angefahamu mambo ya ndani kuhusu kesi zilizokuwa zikiendelea wakati huo.

You can share this post!

Tumepuuzwa na Rais Uhuru, Wapwani walia

Mourinho apokezwa kichapo kinono zaidi katika historia yake...

T L