• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Tumepuuzwa na Rais Uhuru, Wapwani walia

Tumepuuzwa na Rais Uhuru, Wapwani walia

Na MAUREEN ONGALA

BAADHI ya viongozi wa Pwani wamemkosoa Rais Uhuru Kenya kwa kutoangazia changamoto za eneo hilo katika mikakati ya kuinua uchumi aliyotangaza wakati wa sherehe za Mashujaa Dei.

Katika sherehe hizo zilizofanywa Kaunti ya Kirinyaga Jumatano, Rais Kenyatta alitangaza mikakati mingi ya kifedha na sera ikilenga sekta mbalimbali kama vile kilimo, afya, elimu, miundomsingi, kawi, miongoni mwa mengine ili kufufua uchumi wa nchi uliopata pigo kubwa wakati wa janga la corona.

Malalamishi yameibuka kuwa, sekta ya utalii ambayo ni mojawapo ya zile zinazoendelea kupitia hali ngumu zaidi nchini ilisahaulika.

Mwenyekiti wa Baraza la Wahubiri wa Kidini Pwani (CICC), Askofu Amos Lewa, alisema hali hiyo inatoa dhihirisho ya kwamba eneo la Pwani limetengwa kiuchumi.

“Anazidi kuwapa wapinzani na wale wanaokashifu serikali na pia wengine ambao hawana nia njema kwa taifa, nguvu ya kusema Pwani sio sehemu ya Kenya kwa sababu hautuhesabiwi katika masuala ya taifa. Hatujui kama masuala ya Pwani sio muhimu kwake, lakini Rais angeangalia kila eneo nchini,” akasema Bw Lewa ambaye huongoza kanisa la Joy Fellowship Ministries.

Hata hivyo, baadhi ya wadau katika sekta ya utalii walieleza matumaini kuwa hatua ya kuondoa kafyu huenda ikasaidia kibiashara.

Mapema mwaka huu 2021 serikali ililalamika kuwa iliwatengea wawekezaji wa sekta ya utalii Pwani Sh1.8 bilioni mwaka uliopita ili wachukue mikopo ya kufufua biashara zao kwa riba ya chini, lakini wafanyabiashara wakawa walegevu kutuma maombi na Sh300 milioni pekee ndizo zikachukuliwa.

Kando na utalii, viongozi waliolalamika walisema pia ingekuwa bora kama Rais Kenyatta angetaja hatua zinazochukuliwa kufufua sekta muhimu zilizoporomoka kama vile kilimo cha mnazi na mikorosho, na vile vile sekta ya uvuvi ambayo imekumbwa na changamoto ikiwemo kuingiliwa na wavuvi wanaotoka mataifa ya kigeni.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya alisema Pwani imeathirika sana kiuchumi hata kabla ya janga la corona kutangazwa nchini na inasikitisha ikiwa inazidi kusahaulika katika mipango maalumu ya serikali.

“Rais ametuchezea shere. Wapwani wanahitaji msaada wa dharura ili kukomboa uchumi wetu,” akasema.

Kulingana naye, wadau wengi katika sekta ya utalii wangali wanapata hasara kwa vile idadi ya watalii ilipungua sana hadi sasa, ilhali wengine wao walikuwa wanagharamia mikopo.

Alieleza hofu kuwa huenda baadhi ya hoteli hazitafunguliwa kufikia Desemba, na kuna uwezekano ya wafanyakazi wengine wengi kupoteza ajira.

“Sekta ya utalii imeangamia chini ya uongozi wa serikali hii. Tumepoteza pia bandari letu na maelfu ya watu wamepoteza ajira,” akasema.

You can share this post!

DOMO KAYA: Wanasema tabia ni ngozi!

Pigo kwa Gicheru ICC ikikataa ombi lake

T L