• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:10 AM
Raia wa Gaza wapitia mateso ya kutisha hospitali zote zikisitisha huduma

Raia wa Gaza wapitia mateso ya kutisha hospitali zote zikisitisha huduma

NA MASHIRIKA

PALESTINA, GAZA

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA limeonya kwamba bohari yake ya mafuta imekauka na huenda likasimamisha shughuli zake ndani ya saa 48.

Mkuu wa shirika hilo, Thomas White, aliandika kwenye mtandao wa kijamii ya X, “Operesheni zetu huko Gaza huenda zikasimama ndani ya kipindi hicho kwa kuwa hakuna mafuta Gaza.”

White aliongezea kuwa UNRWA imekuwa ikitumia mafuta kutoka hifadhi yake lakini imeishiwa na bidhaa hiyo muhumu kwa kuwa hakuna mafuta yanayoingia Gaza tangu Oktoba 7 wakati Hamas waliposhambulia Israeli.

Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas pia ilisema mapema Jumatatu kwamba hospitali zote kaskazini mwa Gaza hazifanyi kazi tena kutokana na uhaba wa mafuta.

Katika hatua nyingine, Rais wa Amerika, Joe Biden ametoa wito kwa Israeli kuilinda hospitali kubwa ya Al-Shifa katika Ukanda wa Gaza wakati shirika la afya ulimwenguni WHO likisema hospitali hiyo haitoi huduma tena.

Wafanyakazi katika hospitali hiyo wamedai kuzingirwa, baada ya kituo hicho kushambuliwa mara kadhaa kwa mabomu na kuongeza kuwa Israeli inawapiga risasi watu wanaotoka nje ya jengo hilo.

Hata hivyo, Israeli imekanusha madai hayo, ikisema Hamas inatumia mahandaki chini ya hospitali hiyo kushambuliwa wanajeshi wa Israeli, ingawa haijatoa ushahidi wowote kuhusu hilo.

Wakati hayo yakiripotiwa, jeshi la ulinzi la Israeli, IDF, limesema kuwa linaendelea na msako mkali kwenye viunga vya kambi ya wakimbizi ya Al-Shati ndani ya Jiji la Gaza.

IDF ilisema vikosi vyake vilikuwa “vinailenga miundombinu ya kigaidi iliyoko katika taasisi za serikali zikiwemo shule, vyuo vikuu, misikiti na makazi ya magaidi.”

Aidha, taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa kupitia mtandao wa Telegram ilisema wanajeshi wake waliingia kwenye makazi ya mwanachama wa ngazi ya juu wa kundi la Islamic Jihad na kukuta “idadi kubwa ya silaha kwenye chumba cha watoto”.

Islamic Jihad ni kundi dogo la wanamgambo linalofanya oparesheni zake ukanda wa Gaza na lenye mafungamano na Hamas.

Kwa mujibu wa wizara ya Afya inayoongozwa na Hamas, zaidi ya Wapalestina 11,000 wameuawa tangu vita kuanza.

Hapo jana, jamaa wa watu waliotekwa nyara na kundi la Hamas wakati wa mashambulio yake ya Oktoba 7 dhidi ya Israeli, walikusanyika mjini Jerusalem kuushinikiza Umoja wa Mataifa (UN) kuingilia kati suala hilo ili waliotekwa waachiliwe.

  • Tags

You can share this post!

Mafuta ya Sh17bn: Mfanyabiashara asimulia namna alivyoona...

Majengo kadhaa sasa kubomolewa kupisha Jiji Eldoret

T L