• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 3:09 PM
Rais ahepa ghadhabu za raia

Rais ahepa ghadhabu za raia

CHARLES WASONGA NA MASHIRIKA

RAIS wa Sri Lanka Gotabaya Rajapaksa alitoroka Kasri lake Jumamosi kabla ya waandamanaji, waliokerwa na changomoto za kiuchumi, kulivamia na kuharibu mali.

Maelfu ya waandamanaji walizingira makazi hayo rasmi ya kiongozi huyo wakishinikiza kujiuzulu kwake, wakiilaumu serikali yake kwa usimamizi mbaya wa uchumi wa nchi hiyo.

Walitaja udhaifu huo kama chimbuko la kupanda kwa gharama ya maisha uliowafanya kukosa kujikimu kimaisha na madhila mengine yanayowazonga.

Waandamanaji walipokuwa wakikaribia malango ya makazi ya Rais Rajapaksa, walinzi walifyatua risasi angani ili kiongozi huyo aondolewe salama, afisa wa cheo cha juu katika jeshi aliambia shirika la habari la AFP.

“Rais alitolewa ili kumsalimisha,” akasema afisa huyo ambaye aliomba jina lake libanwe.

“Yeye bado ndiye rais, analindwa na kikosi maalum cha wanajeshi,” afisa huyo akaongeza.

Hali kama hiyo imekumba Kenya na mataifa mengine barani Afrika na ulimwengu kwa ujumla.

Kando na utepetevu wa serikali, changamoto hiyo imesababisha na kupanda kwa bei ya mafuta kufuatia hatua ya Urusi kuvamia Ukraine Februari 24, 2022, athari za janga la Covid-19, uhaba wa sarafu za kigeni haswa dola ya Amerika miongoni mwa sababu nyinginezo.

Vita nchini Ukraine na vikwazo ambavyo mataifa ya Magharibi yaliiwekea Urusi, vimevuruga uuzaji nje wa mafuta kutoka Urusi ambalo ni taifa la tatu ulimwenguni kwa uuzaji mafuta.

Aidha, vita hivyo, vimezuia Ukraine kuuza nje nafaka na mafuta ya kupikia ambayo huzalishwa kwa wingi nchini humo.

Naibu Rais William Ruto amelaumu muafaka wa kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenya na kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa tatizo hilo, madai ambayo serikali imekana.

NAIROBI

Mnamo Alhamisi wanaharakati walifanya maandamano katikati mwa jiji la Nairobi wakiwahamasisha raia kususia uchaguzi mkuu wa Agosti 9, ikiwa serikali haitapunguza bei ya bidhaa za kimsingi ndani ya siku 14 zijazo.

Maandamano hayo pia yalifanyika katika mitaa kadha viungani mwa Nairobi na hata mji wa Nyeri, raia wakilalamikia kupanda kwa bei ya unga hadi kuzidi Sh200 kwa paketi moja ya kilo mbili.

Maandamano sawa na hayo yameshuhudiwa wiki hii katika nchini za Afrika Kusini, Zimbabwe, Ghana, Nigeria, Musumbiji, Uganda, Guinea miongoni mwa zingine. Jumatano mtu mmoja aliuawa jijini Conakry kwenye maandamano ya kulalamikia kupanda kwa bei ya mafuta.

Mataifa ya Magharibi kama vile Amerika, Ujerumani, Uingereza, Ubelgiji, Italia miongoni mwa mengine pia hayasazwa na changamoto hiyo. Kwa mfano kwa mara ya kwanza tangi 1981, mfumko wa bei nchini Amerika umefikia kiwango cha asilimia 8.6.

Kufuatia machafuko ya jana Sri Lanka, Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe, aliitisha mkutano wa dharura za baraza la mawaziri kujadili njia za kusuluhisha mzozo huo, afisi yake ilisema.

Kulingana na katiba ya nchi hiyo, kiongozi huyo ndiye atatwaa mamlaka endapo Rais Rajapaksa ataamua kujiuzulu rasmi.

Kwenye picha zilizosambazwa mitandaoni, waandamanaji walionekana wakitembea ndani ya Kasri ya Rais.

Makazi hayo ni mojawapo ya nembo ya mamlaka ya taifa la Sri Lanka.

Baadhi ya maafisa wa serikali walielezea wasiwasi ikiwa Rais Rajapaksa atasalia mamlakani baada ya kutoweka kutoka makazi yake rasmi.

“Tunasubiri maagizo,” afisa wa serikali wa ngazi za juu aliambia AFP.

“Kufikia sasa hatujui mahala ambapo alipelekwa, lakini tunajua kwamba yu salama chini ya ulinzi wa kikosi cha jeshi la wanamanaji,” akaongeza.

Usimamizi wa hospitali kuu jijini Colombo ulisema kuwa watu 14 wanatibiwa humo baada ya kujeruhiwa na mikebe ya gesi za kutoa machozi.

Kwa kipindi cha miezi kadha, taifa la Sri Lanka limezongwa na uhaba wa chakula na mafuta. Aidha, imeshuhudia visa kadha vya kupotea kwa umeme na mfumko wa bei ya bidhaa za kimsingi kutokana uhaba wa sarafu za kigeni kuiwezesha kununua bidhaa za kimsingi kutoka nje.

Maelfu ya watu wamekuwa wakifanya maandamano katika barabara kadha za Colombo kuelezea ghadhabu ya kutokana na madhila hayo.

Polisi waliondoa kafyu iliyotolewa Ijumaa baadhi ya vyama vya upinzani, wanaharakati wa kutetea haki na muungano wa mawakili walipometisha kumshtaki Mkuu wa Polisi.

Awali, maelfu ya waandamanaji walikaidi amri hiyo na hata wakawalazimisha wasimamizi wa shirika la reli kuamuru safari za treni kuwapeleka Colombo kwa mkutano mkubwa, maafisa walisema.

“Kafyu haikudhibiti hali. Watu wengi waliikaidi na kufurika katika barabara za miji,” afisa mmoja wa idara ya jeshi akasema.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Kila mtu ajikinge msimu huu wa baridi

Wazazi, wanafunzi kuendelea kujikaza shule zikifunguliwa

T L