• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Serikali yaahidi uwajibikaji kufuatia shambulio lililoua 21

Serikali yaahidi uwajibikaji kufuatia shambulio lililoua 21

NA AFP

MOGADISHU, SOMALIA

WAZIRI Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Barre ameahidi uwajibikaji kutoka kwa serikali yake kufuatia kisa ambapo magaidi wa Al-Shabaab walishambulia mkahawa mmoja na kuua watu 21.

Aidha, amewataka raia wa Somali kuungana dhidi ya wanamgambo hao ambao wamekuwa wakiendeleza mashambulio nchini humo kwa miaka 15 iliyopita.

“Kutakuwa na uwajibikaji katika serikali. Mtu yoyote ambaye alitelekeza wajibu aliopewa atalazimishwa kuwajibika. Kuna chaguo mbili pekee hapa: ama turuhusu Al-Shabaab – watoto wa jehanamu – waishi au sisi tuishi. Hatuwezi kuishi pamoja na wahalifu hawa,” akasema Barre, aliyeteuliwa mnamo Juni 2022.

Waziri mkuu alikuwa akiongea Jumatatu jioni baada ya kuwatembelea waathiriwa wa shambulio hilo dhidi ya mkahawa wa Hayat katikati wa jiji la Mogadishu.

Jumla ya watu 117 walijeruhiwa katika shambulio hilo lililotekelezwa mnamo Ijumaa jioni.

Maafisa wa serikali walisema zaidi ya watu 100, wakiwemo wanawake na watoto, waliokolewa baada ya magaidi hao kuwateka wateja waliokuwa ndani ya hoteli kwa saa 30.

Shambulio hilo ndilo baya zaidi kutokea nchini Somalia tangu Rais Hassan Sheikh Mohamud aliyechaguliwa mnamo Mei 2022.

Hii ni baada ya Somalia kushuhudia mvutano wa kisiasa uliodumu kwa muda.

Wapiganaji wa Al-Shabaab walivamia mkahawa huo Ijumaa na kudhibiti hadi Jumamosi usiku baada ya wanajeshi wa Somalia kushambulia jengo hilo na kuharibu kuta zake.

Maafisa wa serikali hupenda kufanya mikutano katika hoteli hiyo ya Hayat na wageni wengi walikuwa humo mshambuliaji wa kujitoa mhanga alipotekeleza shambulio la kwanza.

Baadaye watu wenye bunduki waliingia ndani ya mkahawa huo na kufanya mashambulio ya risasi.

Muda mfupi baadaye, mlipuko wa pili ulitokea wakati ambapo waokoaji, maafisa wa usalama, na raia walifika hapo kuwasaidia waliojeruhiwa.

Wapiganaji wa Al-Shabaab wametekeleza mashambulio kadhaa tangu Rais Mohamud alipoingia mamlakani.Mwezi uliopita wanamgambo hao waliingia katika taifa jirani la Ethiopia na kushambulia kambi moja ya wanajeshi eneo la mpakani.

Mapema mwezi Julai, Amerika ilisema wanajeshi wake waliuawa wapiganaji 13 wa Al-Shabaab kwa kufanya shambulio la angani.

Hilo lilikuwa shambulio la kwanza tangu Rais wa Amerika Joe Biden kuwarejesha wanajeshi wa Amerika nchini Somalia.

Mtangulizi wake, Donald Trump, aliwaondoa wanajeshi wa Amerika nchini Somalia mnamo 2019.

Wapiganaji wa Al-Shabaab waliondolewa jijini Mogadishu na muungano wa wanajeshi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika (Amisom) mnamo 2011.

Hata hivyo, wanamgambo hao bado wanadhibiti maeneo kubwa ya mashambani nchini Somalia.

Aidha, wamekuwa wakifanya mashambulio katika mikahawa pamoja na vituo vya kijeshi na kisiasa.

Mnamo Oktoba 2017 Al-Shabaab walitekeleza shambulio baya zaidi jijini Mogadishu ambapo lori lililojaa vilipuzi lililipuka na kuwaua watu 512.

  • Tags

You can share this post!

Demokrasia yazidi kunawiri Kenya, asema mkurugenzi wa MPC

Raila aambiwa mwenyekiti IEBC hasimamii uchaguzi wa ugavana

T L