• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
SULUHU APATA MPANGO TZ

SULUHU APATA MPANGO TZ

NA MASHIRIKA

RAIS mpya wa Tanzania Samia Suluhu alimteua Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Isdor Mpango kuwa makamu wake. Waziri huyo sasa ataapishwa Jumatano saa tisa alasiri kama Makamu mpya wa Rais baada ya kuidhinishwa bila kupingwa na Bunge la Tanzania.

Rais Suluhu alipendekeza jina la Mpango lililowasilishwa bungeni Jumanne asubuhi.

Spika wa Bunge, Bw Job Ndugai, alitangaza jina hilo ambapo asilimia 100 ya wabunge wote 363 walipiga kura kumwidhinisha Mpango.

Akizungumza baada ya kuidhinishwa kwake na Bunge hilo la 12 nchini Tanzania, Waziri huyo wa Fedha alieleza jinsi alivyopigwa na butwaa kufuatia uteuzi wake ambao hakuutarajia.

“Ningependa kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri jeshi mkuu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kupendekeza jina langu.Hii ni nafasi muhimu sana na nyeti. Kuwa makamu wa rais ni heshima kubwa sana ambayo sikuwahi kuota, nimepigwa na butwaa.”

Dkt Mpango ambaye ana Shahada ya Uzamifu katika Taaluma ya Uchumi, aliahidi kutimiza ndoto ya marehemu Rais John Pombe Magufuli na kubadilisha uchumi wa Tanzania kuwa wa kiwango cha juu.

“Jambo muhimu na la haki tunaloweza kumtendea ni kutimiza ndoto yake. Ni lazima tuibadilishe Tanzania, lazima tusimamie rasilimali za nchi yetu.”

“Ningependa sana tuimarike kutoka nchi yenye kipato cha chini na kuwa nchi yenye kipato cha juu haraka na inawezekana tukiamua kwa pamoja kama Watanzania,” alisema Dkt Mpango.

Kulingana na katiba ya Tanzania, ni sharti jina lililopendekezwa na rais liungwe mkono na asilimia 50 ya wabunge ili kuidhinishwa.

Jina la Dkt Mpango lilikuwa kwanza limewasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu ya chama tawala cha CCM ili kuidhinishwa, kabla ya kuwasilishwa bungeni ili nalo lifanye uamuzi wake.

Wakati huo huo, polisi nchini Tanzania walisema jana kuwa watu 45 walifariki katika mkanyagano jijini Dar-es-Salaam, mnamo Machi 21, waombolezaji walipokuwa wakimpa heshima ya mwisho hayati Rais Magufuli.

Mkanyagano huo ulitokea wakati maelfu ya raia waliokuwa wakiomboleza, walipokuwa wakisukumana kuingia uwanjani kumuaga kiongozi wao.

“Kulikuwa na watu wengi mno waliotaka kuingia uwanjani, na baadhi hawakuwa na subira. Walijaribu kuingia ndani kwa kifua na kusababisha mkanyagano. Watu 45 walifariki katika ajali hiyo,” Kamanda wa Polisi Dar es Salaam, Bw Lazaro Mambosasa alieleza vyombo vya habari.

Kifo cha Magufuli kilitangazwa Machi 17 baada ya kutoweka kwa muda katika hali iliyozingirwa na utata.

You can share this post!

Hii kafyu inaumiza wananchi – Kalonzo

Shaffie Weru sasa afukuza Sh21 milioni akidai alipigwa...