• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Tutazungumza na Al-Shabaab kwa wakati mwafaka, asema Rais wa Somalia

Tutazungumza na Al-Shabaab kwa wakati mwafaka, asema Rais wa Somalia

NA AFP

MOGADISHU, SOMALIA

RAIS mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud sasa anasema kuwa serikali yake ifanya mazungumzo na kundi la wapiganaji wa Al-Shabaab ila kwa “wakati ufaao”.

Alisema hatua hiyo ni mbinu mbadala kukomesha mashambulio ya wafuasi wa kundi hilo kando na mbinu ya kijeshi.

Rais Mohamud ambaye alichaguliwa mnamo Mei 2022 alisema kundi hilo, limebuni mikakati ya maalum ya “kustahimili” makali kutoka kwa wanajeshi na haliwezi kudhibitiwa kwa nguvu pekee.

“Wakati huu hatuko tayari kufanya mazungumzo na Al-Shabaab. Tutafanya hivyo wakati utakaofaa,” Rais Mohamud akaambia kundi la wataalamu wakati wa ziara yake nchini Uturuki wiki hii.

“Hata wakati huu… tutawakubali wale ambao wameamua kuachana na vita, itikadi kali, na wanataka kurejelea maisha ya kawaida nchini Somalia,” akaongeza.

Rais Mohamud alisikitika kwamba mbinu za awali za kupambana na Al-Shabaab hazijafanikiwa.

Alihudumu kama Rais kati ya mwaka wa 2012 na 2017.

Kwa muda wa mwongo mmoja kundi la Al-Shabaab limekuwa likitekeleza mashambulio nchini Somalia kwa lengo la kuindoa mamlakani serikali ya sasa inayoungwa mkono na mataifa ya kigeni.

Wafuasi wa kundi hilo, lenye uhusiano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda, wamesalia kuwa tishio kwa serikali ya Somalia licha ya juhudi za kuwalemea kwa kutumia wanajeshi.

Mnamo mwaka wa 2011 wapiganaji wa Al-Shabab walifurushwa kutoka jiji kuu la Mogadishu na wanajeshi wa Umoja wa Afrika (AU).

Hata hivyo, wafuasi wa kundi hilo wangali wanadhibiti maeneo makubwa ya mashambani ambako wao hutekeleza mashambulio dhidi ya raia na vituo vya wanajeshi.

Rais Mohamud alisema japo serikali zilizopita zilitekeleza sera ya kukabiliana na Al-Shabaab kijeshi kwa kuharibu vituo vyao, “wameweza kuunda vituo vipya”.

“Wameweza kurejea katika uwanja wa vita tena,” akasema.

Kiongozi huyo ambaye ni msomi na mwanaharakati za kutetea amani, alisema mbinu nyingine ya kulemaza Al Shabaab ni kukatizwa kwa njia ambazo kundi hilo hutumia kupata fedha na kujibu jumbe zao za chuki.

Baada ya kuchaguliwa kwake, Mohamud aliunga mkono tangazo la Rais wa Amerika Joe Biden kwamba serikali itarejesha wanajeshi nchini Somalia.

Mnamo 2019, mtangulizi wa Biden, Donald Trump aliwaondoa wanajeshi wa Amerika kutoka Somalia akisema serikali yake haikuwa tayari kuendelea kupambana na Al Shabaab.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Wawaniaji huru wajiepushe na kampeni kunadi...

Man-Utd yamtega staa Antony na Sh7.2 bilioni

T L