• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
Ujumbe wa UN kukagua kituo cha nyuklia Ukraine

Ujumbe wa UN kukagua kituo cha nyuklia Ukraine

NA MASHIRIKA

NEW YORK, AMERIKA

UMOJA wa Mataifa (UN) umetuma kikosi maalum kuchunguza na kufuatilia hali inavyoendelea katika Kituo cha Nyuklia cha Zaporizhzhia, nchini Ukraine.

Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Kawi ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi, alisema kikosi hicho kinatarajiwa kufika katika kituo hicho baadaye wiki hii.

“Lazima tuhakikishe kuwa hali ya usalama imedumishwa katika kituo hicho, kwani ndicho kikubwa zaidi nchini Ukraine na bara Ulaya kwa jumla. Ni muhimu kuhakikisha mapigano yanayoendelea hayasababishi miale hatari inayoweza kuiathiri dunia,” akasema.

Kituo hicho kimekuwa kikidhibitiwa na majeshi ya Urusi tangu walipokiteka mnamo Machi.

Hata hivyo, mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea karibu na kituo hicho yamezua wasiwasi duniani, kwamba huenda “mlipuko” wa miale yake ukaleta madhara makubwa duniani.

Urusi na Ukraine zimekuwa zikilaumiana kwa kukishambulia kituo hicho.

Hakuna upande wowote uliokubali ndio unafanya mashambulio dhidi yake. Mnamo Alhamisi, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alisema bara Ulaya limo karibu sana kuathiriwa na mlipuko wa miale hatari ya nyuklia, baada ya kituo hicho kutenganishwa kwa muda na mfumo wa kusambaza umeme.

Jeshi la Urusi lilichukua udhibiti wa kituo hicho mapema mwezi Machi, ijapokuwa shughuli zake bado zinaendeshwa na raia wa Ukraine, japo katika mazingira magumu.

Awali, Urusi ilisema itawaruhusu wachunguzi wa kimataifa kuzuru kituo hicho, ili kubaini yale yanayoendelea.

Kwa upande wake, Ukraine ilieleza wasiwasi wake kuwa ziara ya ujumbe wa IAEA itazua taswira kwamba Urusi inakidhibiti kituo hicho kwa njia halali.

“Karibu kila siku, kuna kisa kipya katika au karibu na Kituo cha Nyuklia cha Zaporizhzhia. Hatutaendelea kupoteza muda bila kufahamu yanayoendelea,” ikasema IAEA kwenye taarifa.

Wataalamu wa masuala ya nyuklia hata hivyo wanasema kuwa kushambuliwa kwake hakupaswi kuzua wasiwasi sana, kwani kina kuta zenye nguvu kukisaidia kuhimili mashambulio dhidi yake.

Wanaeleza kuwa kile kinachopaswa kuzua wasiwasi ni kukatwa kwa umeme mara kwa mara.

“Ni hali hatari inayoweza kusababisha mlipuko wa kemikali zilizohifadhiwa kwenye matangi tofauti,” ikaeleza IAEA.

Wakati huo huo, Waziri wa Kawi nchini Ubelgiji, Tinne Van der Straeten, ameonya kuwa huenda mataifa ya Ulaya yakaathiriwa vibaya na msimu wa baridi kutokana na bei ya juu ya gesi.

Mataifa ya Ulaya yamekuwa yakikabiliwa na uhaba mkubwa wa gesi tangu Urusi kuivamia Ukraine mnamo Februari. Mataifa hayo huwa yanayategemea pakubwa nchi hizo mbili kupata gesi.

Urusi huwa inauza asilimia 40 ya gesi yake nchini Ulaya. Hata hivyo, ilipunguza mauzo yake baada ya mataifa hayo kuiwekea vikwazo vya kiuchumi.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Serikali iwe makini kuzingatia ushauri wa...

Malala akubali kushindwa akipongeza IEBC kwa kazi nzuri

T L