• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
UN yatakiwa kuadhibu China kwa kukiuka haki

UN yatakiwa kuadhibu China kwa kukiuka haki

NA MASHIRIKA

WANADIPLOMASIA pamoja na watetezi wa haki za binadamu, wameongeza shinikizo kwa Umoja wa Mataifa (UN) kuchukua hatua dhidi ya China kwa kudhulumu watu wa kabila la Uighur pamoja na makundi mengine ya Waislamu.

Miito ya hatua dhidi ya China imeongezeka huku viongozi wa mataifa mbalimbali duniani wakikusanyika katika makao makuu ya UN jijini New York, Amerika kwa Kongamano Kuu la UN (UNGA).

Wiki mbili zilizopita, Tume ya UN kuhusu Haki za Binadamu ilitoa ripoti ambayo ilisema China inakiuka haki za binadamu katika mkoa wake wa Xinjiang.

Fernand de Varennes, ambaye ni balozi maalum wa UN kuhusu haki za watu wa makabila madogo, alisema iwapo hakuna hatua itachukuliwa dhidi ya China, umoja huo utakuwa unatuma ujumbe usiofaa duniani.

Naibu balozi wa Amerika katika UN, Jeffrey Prescott aliunga mkono kauli hiyo akisema uwajibikaji wa UN utakuwa kwenye hatari China isipochukuliwa hatua.

“Vile suala hili litashughulikiwa itaonyesha hali halisi ya mfumo wa kimataifa. Inasikitisha kuona moja ya mataifa yaliyotekeleza wajibu mkubwa kubuni mfumo wa UN likikaidi kanuni zake,” akasema Prescott.

Tangu 2018 kumekuwa na ripoti kuhusu ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu mkoani Xinjiang, ambako watu wa kabila la Uighur wamedhulumiwa kwa kufungiwa kwenye kambi, kufanyishwa kazi kwa lazima, familia kutenganishwa na kuharibiwa kwa utamaduni na imani zao za kidini.

China ilikiri kuwepo kwa kambi hizo, lakini ikadai ni vituo vya kuwapa mafunzo ya kikazi watu wa kabila la Uighur katika juhudi za kuzuia itikadi kali za kidini.

Wakati UN ilipotoa ripoti kuhusu dhuluma mkoani Xinjiang, China iliipinga vikali ikidai ulikuwa ni uwongo wa mataifa ya magharibi.

Kwa sasa taifa hilo linaendeleza kampeni ya kutafuta uungwaji mkono ili kuzuia UN kulichukulia hatua, ikilenga zaidi kuungwa mkono na mataifa ambayo imekuwa ikisaidia kifedha pamoja na maadui wa Amerika.

Ripoti ya kwanza ilipotolewa Agosti 31, wanadiplomasia wa China walitoa ripoti waliyosema iliungwa mkono na mataifa mengine 30 yakiwemo Urusi, Korea Kaskazini, Saudi Arabia na Venezuela wakipuzilia mbali madai ya ukiukaji haki Xinjiang.

Wakati huo huo, UN inatarajiwa kujadili mizozo inayokumba maeneo mengi duniani pamoja, mabadiliko ya hali ya anga na kupanda kwa gharama ya maisha katika mataifa mengi duniani.

Kikao cha mwaka huu cha UNGA kinatarajiwa kuangazia zaidi mzozo baina ya Urusi na Ukraine, ambao umelaumiwa kwa kuchangia kupanda kwa bei ya gesi, petroli na nafaka kote duniani.

  • Tags

You can share this post!

Kilifi kubadili siasa za Pwani – Wachanganuzi

Kaunti yasambaza chakula cha msaada kwa familia elfu 20

T L