• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
UN yatoa tahadhari, njaa kutesa Sudan

UN yatoa tahadhari, njaa kutesa Sudan

NA XINHUA

KHARTOUM, SUDAN

UMOJA wa Mataifa (UN) kwa mara nyingine umeonya kuhusu uwezekano wa Sudan kushuhudia uhaba mkali wa chakula baada ya kukatizwa kwa ufadhili kutoka mataifa ya ng’ambo.

“Ukosefu wa chakula na mahitaji mengine ya kimsingi unasalia kuwa changamoto kuu nchini Sudan. Raia wengi wanaendelea kuhama makwao huku wakimbizi wakiendelea kuwasili kutoka mataifa jirani hasa Sudan Kusini, Ethiopia na Eritrea,” afisi ya Umoja wa Mataifa ya Kushirikisha Masuala ya Utoaji Misaada ya Kibinadamu (OCHA) ikasema katika ripoti yake ya hivi punde.

“Inakadiriwa kuwa karibu robo ya watu nchini Sudan (sawa na watu 11.7 milioni) watakabiliwa na makali ya njaa kuanzia Juni hadi Septemba mwaka huu. Hii ni sawa na ongezeko la karibu watu millioni mbili ikilinganishwa na wakati kama huo mwaka jana,” OCHA ikasema huku ikinukuu uchanganuzi uliofanywa na shirika la Integrated Food Security Phase Classification (IPC) kuhusu utoshelevu wa chakula nchini Sudan.

Wakati huo huo, Shirika la Chakula Ulimwenguni (WFP) nchini Sudan limetangaza kuwa limelazimika kupunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi nchini humo tangu Juni, kutokana na uhaba wa ufadhili, OCHA ikasema katika ripoti yake.

WFP husaidia zaidi ya wakimbizi 550,000 nchini Sudan kila mwaka, wakiwemo raia waliofurushwa makwao kutokana na vita, ripoti hiyo ikaongeza.

Shirika hilo linaelezea hofu kuwa kukatizwa kwa ufadhili wa kigeni kwa mpango wake wa utoaji chakula kunaweza kuchangia wakimbizi kuingilia maovu kama ajira ya watoto, ndoa za mapema, ukahaba, watoto kuacha shule, dhuluma za kimapenzi miongoni mwa mengine.

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Chakula (FAO) lilisema ongezeko la watu wanaokabiliwa na baa la njaa nchini Sudan limesababishwa na kuzorota kwa uchumi, kiangazi cha muda mrefu, kupungua kwa mashamba yanayotumika kwa ukuzaji wa chakula na uhaba wa mvua, inasema ripoti hiyo ya OCHA.

FAO imezindua mradi mpya unaolenga kuongeza uzalishaji wa chakula miongoni mwa jamii za wakulima na wafugaji kupitia mpango wa usambazaji wa mahitaji ya kufanikisha shughuli hizo, ripoti hiyo inaongeza.

Sudan imekuwa ikishuhudia ongezeko la bei ya mkate, unaookwa kutokana na unga wa ngano, huku bei hiyo ikifika hadi Dola 0.11 (Sh13).

Hali hii imechangiwa na kupungua kwa uzalishaji wa ngano nchini humu kutoka asilimia 70 ya mahitaji ya kitaifa kwa mwaka hadi asilimia 60.

Kulingana na takwimu kutoka kwa serikali, Sudan huhitaji tani milioni 2.4 za ngano kila mwaka lakini uzalishaji ulipungua hadi tani 700,000 mwaka 2021.

  • Tags

You can share this post!

Ruto alalama kuhusu njama ya kuiba kura

WANDERI KAMAU: Kudhulumu wahudumu ni kosa, adhabu yake ni...

T L