• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Ruto alalama kuhusu njama ya kuiba kura

Ruto alalama kuhusu njama ya kuiba kura

NA LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto jana Alhamisi alitoa msururu wa malalamishi akidai kunyanyaswa na kuwepo kwa njama ya wapinzani wake kufanya udanganyifu katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Dkt Ruto alidai watumishi wa umma wanatumiwa katika mpango huo wa wizi wa kura.

Katika orodha yake ya maafisa wa serikali anaowashuku kuhusika na udanganyifu, ni Waziri wa Teknolojia ya Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mawasiliano (CA) Ezra Chiloba, Kamishna wa Kanda ya Bonde la Ufa Maalim Mohamed, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kusambaza Umeme nchini (Kenya Power) Geoffrey Muli, machifu na manaibu wao.

Naibu wa Rais anashuku Bw Chiloba ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na Bw Mucheru huenda wakatumia mamlaka yao kutatiza intaneti hivyo kuathiri upeperushaji wa matokeo siku ya uchaguzi.

Mnamo Alhamisi, Dkt Ruto aliyekuwa akihutubia wanahabari wa kimataifa na humu nchini katika makazi yake mtaani Karen, Nairobi, alielezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kampuni ya Kenya Power kuzima umeme kote nchini siku ya uchaguzi.

“Bw Chiloba na Bw Muli ni sharti watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa sheria. Hatutaki kuona intaneti au umeme ukizimwa kama walivyofanya siku ya mjadala wa urais; ni kinyume cha sheria,” alisema Dkt Ruto.

Jumatano, kinara mwenza wa Kenya Kwanza Moses Wetang’ula (Ford Kenya) alidai Waziri Mucheru anaendelea na mikakati ya kuweka mtambo utakaotatiza intaneti katika baadhi ya maeneo nchini Jumanne.

Aidha, Naibu wa Rais alidai Bw Maalim amekuwa akifanya mikutano ya usiku kupanga kuzua vurugu siku ya uchaguzi kwa lengo la kuzuia wakazi wa Bonde la Ufa ambayo ni ngome yake kujitokeza kupiga kura.

Alidai Bw Maalim anasaidiwa kufanya njama hiyo na makamishna Samson Ojwang wa Trans Nzoia na Erastus Mbui wa Nakuru.

Naibu wa Rais alidai Rais Uhuru Kenyatta anafahamu kuhusu mikutano hiyo ambayo imekuwa ikifanywa usiku katika Kaunti ya Nakuru.

“Rais anafahamu mipango hiyo na tunamsihi kuwazuia mara moja ili wasizue mapigano,” akasema Dkt Ruto.

Alihusisha mikutano hiyo ya usiku na vijikaratasi vya chuki vilivyokuwa vikisambazwa hivi majuzi katika baadhi ya maeneo ya Kaunti ya Uasin Gishu.

Lakini Bw Maalim jana Alhamisi aliambia Taifa Leo kuwa, hana habari kuhusiana na mipango hiyo ya kutaka kuzua vurugu.

Dkt Ruto pia alishambulia baadhi ya vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo kwa lugha ya Kikuyu (Inooro na Kameme) kwa madai ya kuchochea chuki.

Alidai wabunge wa zamani Bw Njenga Mungai (Molo) na Bw Joseph Kiuna (Njoro) wamekuwa wakieneza chuki kupitia vituo hivyo vya redio.

Dkt Ruto ambaye anawania urais kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA) pia alionekana kufokea IEBC licha ya kujitokeza kutetea tume hiyo hivi majuzi iliposhutumiwa na wapinzani wake wa Azimio.

Alisema mrengo wake wa Kenya Kwanza utaandikia tume hiyo barua kuitaka kurekebisha baadhi ya mambo ambayo alidai huenda yakatoa mwanya kwa wapinzani kuiba kura.

“IEBC ni sharti itekeleze majukumu yake kwa kuzingatia sheria ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki. Hatutaki kupendelewa ila tunataka uchaguzi uwe wazi,” akasema.

Kulingana na Naibu wa Rais, machifu na manaibu wao wameunda vikundi vya watu watakaokuwa wakitoa hongo katika vituo vya kupigia kura kote nchini Jumanne ili kumfaa mpinzani wake mkuu Bw Raila Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance.

“Machifu, manaibu na watumishi wengine wa serikali wakatae kutumiwa kutatiza uchaguzi kwani kazi zao zimelindwa na Katiba na hawatafukuzwa wakikataa,” akabainisha.

Aidha, Dkt Ruto alishutumu serikali kwa ‘kunyanyasa’ viongozi wa Kenya Kwanza ambao alisema wamekuwa wakizuiliwa kuandaa mikutano kwenye viwanja mbalimbali nchini kwa lengo la kufifisha kampeni zao.

Alitaja kisa cha Jumatatu ambapo Naibu wa Rais pamoja na vinara wenzake wa Kenya Kwanza; Musalia Mudavadi (ANC) na Seneta wa Bungoma Wetang’ula walizuiliwa kufanya mkutano wao ndani ya uwanja wa Bukhungu, Kaunti ya Kakamega.

“Leo (jana Alhamisi) tunafaa kuwa na mkutano wetu wa mwisho katika uwanja wa Tononoka, Mombasa. Lakini tumeambiwa kuwa mkutano hautakuwepo kwa sababu Rais Uhuru Kenyatta atakuwa Mombasa. Nani alisema kuwa Rais akiwa Mombasa hatufai kuwa na mkutano uwanjani Tononoka? Visingizio vya aina hii havifai,” alisema Dkt Ruto.

Rais Kenyatta yuko ziarani jijini Mombasa ambapo jana alizindua Daraja Makupa Bridge lililojengwa kwa Sh4.5 bilioni.

Dkt Ruto alitoa malalamishi hayo muda mfupi baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Joseph Sergon kuagiza muungano wa Kenya Kwanza kufanyia mkutano wao wa mwisho Jumamosi katika uwanja wa Nyayo, Nairobi.

Katibu Mkuu wa UDA Veronica Maina alienda kortini baada ya halmashauri ya kusimamia viwanja vya michezo, Sports Kenya, kuzuia Kenya Kwanza kufanyia mkutano wao wa kisiasa uwanjani Nyayo.

Uwanja huo umekuwa ukizozaniwa kati ya muungano wa Azimio na Kenya Kwanza.

Baadaye, muungano wa Azimio ulibadili nia na kutangaza kuandaa mkutano wake wa mwisho katika Uwanja wa Kasarani.Viongozi wa Kenya Kwanza walikuwa wametishia kufanyia mkutano katikati mwa jiji la Nairobi endapo wangezuiliwa kuingia uwanjani Nyayo- hali ambayo ingetatiza shughuli za usafiri.

Aidha, Dkt Ruto pia alipuuzilia mbali ripoti za utafiti wa kura za maoni ambazo zimetabiri kuwa Bw Odinga ana nafasi nzuri ya kushinda urais Jumanne.

“Serikali imechelewa kufanya njama ya kuiba kura ili kufaa ‘mradi’ wao (Bw Odinga). Hata wakifanya tafiti za kura ya maoni kila siku bado tutawashinda,” akasema Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Raila ashinda kesi kuhusu utumizi wa daftari

UN yatoa tahadhari, njaa kutesa Sudan

T L