• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
WANDERI KAMAU: Kudhulumu wahudumu ni kosa, adhabu yake ni kali!

WANDERI KAMAU: Kudhulumu wahudumu ni kosa, adhabu yake ni kali!

NA WANDERI KAMAU

WIKI iliyopita, msanii mcheshi Timothy Njuguna, maarufu kama ‘Njugush’ alisimulia kisa ambapo mmiliki wa hoteli alimkaripia vikali na kumpiga mmoja wa wafanyakazi wake hadharani.

Kisa hicho kilifanyika katika moja ya hoteli maarufu jijini Nairobi, ambayo nyakati zote huwa na idadi kubwa ya wateja.

Cha kusikitisha ni kuwa, kando na kukaripiwa, mfanyakazi huyo alifutwa kazi muda mfupi baada ya kisa hicho.

Kulingana na mcheshi huyo, ‘kosa’ kuu alilofanya mfanyakazi huyo ni kuwachelewa kupelekea baadhi ya wateja chakula walichokuwa wameagiza.

Bila shaka, simulizi hiyo inaashiria taswira na uhalisia uliopo katika maeneo mengi ya kufanyia kazi nchini.

Ingawa mwanadamu ameumbwa kwa mfano wake Mwenyezi Mungu, amejigeuza mbaya hata kuliko Shetani.

Maeneo ya kufanyia kazi yamegeuzwa majukwaa ya ufisadi, mapendeleo, ngono, ukabila na kila aina ya maovu.

Wakubwa huwa wanatumia ushawishi kuwapandisha ngazi marafiki wao, bila kuzingatia tajriba au weledi wa wafanyakazi waliopo.

Kwa wanawake, imekuwa kawaida kwao kuajiriwa au kupandishwa ngazi baada ya kushiriki ngono na wakubwa wao.Taratibu za uajiri pia zimekuwa zikizingatia ukabila, au “ukaribu” wa mwajiri na mwajiriwa.

Bila shaka, maovu haya hayamo kwenye sekta ya hoteli pekee, bali yamekita mizizi serikalini na hata sekta ya kibinafsi.

Kando na maovu hayo, imeibuka pia kwamba, baadhi ya hoteli zimekuwa zikiwabagua Waafrika kwa kuonekana kuwa “viumbe duni..”

Visa hivi vimekuwa vikiripotiwa hasa katika maeneo ya Pwani na miji mikubwa kama Nairobi, Mombasa, Kisumu na Nakuru, ambako watalii huenda katika hoteli hizo kula na kutafuta malazi.

Majuzi, iliwalazimu wamiliki wa hoteli moja jijini Nairobi kuomba radhi, baada ya video kusambazwa mitandaoni ikionyesha baadhi ya wasimamizi wake wakiwabagua Watu Weusi waziwazi.

Kwa kweli, matukio haya ni ya kusikitisha. Ni visa vinavyoturejesha katika karne ya 19, wakati Waarabu na Wareno walikuwa wakiivamia Afrika na kuwateka Waafrika, kisha baadaye kuwauza katika sehemu tofauti duniani kama watumwa.

Ni mtindo uliowafanya baadhi ya Waafrika-Waarabu maarufu kama Tippu Tip kutoka kisiwa cha Zanzibar kubuni masoko ya kuwauzia watumwa.

Kama nchi huru, iliyojinyakulia uhuru wake kutoka kwa Uingereza mnamo 1963, visa kama hivi havipaswi kujitokeza kamwe.

Ujumbe kwa wanaowabagua, kuwatesa, kuwadunisha na kuwadhulumu wanadamu wenzao: Kuna Mungu awateteao watu wake. Kuna Mungu wa watu maskini. Mtajutia vitendo vyenu.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

UN yatoa tahadhari, njaa kutesa Sudan

CECIL ODONGO: Madai ya Ruto, Amerika yanalenga kusawiri...

T L