• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 2:24 PM
Urusi yalipiza kwa vikwazo vya Biden

Urusi yalipiza kwa vikwazo vya Biden

NA MASHIRIKA

KYIV, UKRAINE

URUSI Jumamosi ilichapisha majina ya watu 963 maarufu kutoka Amerika, ambao imewapiga marufuku kusafiri nchini humo.

Hatua hiyo inaonekana kama ulipizaji kisasi baada ya Amerika kuchukua hatua kama hiyo.

Miongoni mwa watu walio kwenye orodha hiyo ni Rais Joe Biden, mmiliki wa mtandao Facebook Mark Zuckerberg na mwigizaji Morgan Freeman.

Watu wengine walio kwenye orodha hiyo ni maafisa wakuu wa serikali ya Amerika na wabunge.Orodha hiyo ilitolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Urusi.

Tayari, Urusi ilikuwa imewawekea vikwazo baadhi ya watu walio kwenye orodha hiyo kama vile Biden, Waziri wa Mashauri ya Kigeni Anthony Blinken, msimamizi wa makao makuu ya jeshi ya Pentagon, Lloyd Austin na Zuckerberg.

Ijapokuwa Freeman hakuwa amewekewa vikwazo, maafisa wa serikali wa Urusi wanamlaumu kwa kurekodi video mnamo 2017, ambapo alidai kuwa Urusi ilikuwa ikipanga njama dhidi ya Amerika.

“Vikwazo hivyo ni muhimu ili kuidhihirishia Amerika kuwa haitaendelea kuidhibiti dunia itakavyo. Hatutairuhusu kuturejesha katika enzi ya giza,” ikaeleza Urusi kwenye taarifa.

Hata hivyo, Urusi ilisema iko tayari kushiriki mazungumzo ya wazi ili kutatua mvutano kati yake na Ukraine.

Urusi inawalaumu watu hao kwa kuendeleza uchochezi dhidi yake duniani.

Tangu Urusi kuanza mashambulio yake dhidi ya Ukraine mnamo Februari, Urusi imewapiga marufuku mamia ya watu wanaoonekana kuiunga mkono Ukraine kwenye vita hivyo.

Urusi pia imesema imewapiga marufuku raia 26 wa Canada dhidi ya kusafiri nchini humo.

Miongoni mwa raia hao ni mkewe Waziri Mkuu Justin Trudeau, Sophie Trudeau.

Wakati huo huo, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema taifa hilo liko tayari kuikabidhi Urusi watu inaowazuilia ili Urusi kuikabidhi wanajeshi wake waliojisalimisha kwake katika kiwanda cha kutengeneza chuma cha Azovstal, jijini Mariupol.

Zelensky alisema lengo lake kuu ni kuwaokoa raia na wanajeshi wa taifa hilo kwa njia yoyote atakayoweza.

“Tutawarejesha wote nyumbani,” akasema.

Urusi inadai kuchukua udhibiti kamili wa Mauripol, baada ya kundi la mwisho la wanajeshi wa Ukraine kujisalimisha.Zelensky alisema kuwa Ukraine itafanya lolote iwezalo kumaliza mapigano hayo, ambayo yalianza Februari.

Mapigano hayo yamesababisha maafa ya maelfu ya watu, huku wengine 6.3 milioni wakiachwa bila makao au kutorokea katika nchi jirani.

Alisema kuwa mazungumzo ndiyo njia ya pekee ya kumaliza vita hivyo.

“Tutapata suluhisho kamili la mzozo huu kupitia mazungumzo,” akasema.

Kwingineko, mapigano makali yaliendelea kushuhudiwa jana katika eneo la Severodonetsk, huku Urusi ikiendelea na juhudi za kutwaa eneo la Luhansk.

Gavana wa eneo hilo, Serhiy Haidai, alisema vikosi hivyo vinaendelea “kufanya uharibifu mkubwa” katika mji wa Severodonetsk.

Kwenye ujumbe aliotoa kwenye mtandao wa Telegram, alisema kuwa wanajeshi wa Ukraine walifanikiwa kuzima mashambulio 11.

Alisema vifaru vinane vya Urusi na magari kadhaa yaliharibiwa. Hata hivyo, madai hayo hayakuthibitishwa.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Wakenya walioko katika kambi za IDPs wadi...

Washirika wa Raila Magharibi wamrai Kalonzo kurudi Azimio

T L