• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Vibanda vya mahasla vyabomolewa, ziara ya Papa Francis ikikaribia

Vibanda vya mahasla vyabomolewa, ziara ya Papa Francis ikikaribia

NA REUTERS

KINSHASHA, DRC CONGO

VIBANDA vikuukuu vya wafanyabiashara vilivyo katikati mwa jiji la Kinshasha, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, vimeanza kubomolewa ziara ya Papa Francis nchini humo ikikaribia.

Maafisa wa polisi walikuwa katika harakati za kufanya usafi wakiwa na viunzi na tingatinga.

Papa Francis anatarajiwa kufika katika nchi hiyo Januari 31.

Maafisa wanasema Kinshasa, jiji kubwa maskini lenye watu milioni 17, linasafishwa sio tu kwa ajili ya kumuenzi Papa Francis bali kufanya mitaa na barabara zake kuwa safi na zenye utaratibu zaidi hata baada ya kuondoka kwake.

Lakini wafanyabiashara wadogo waliotimuliwa kwenye vibanda vyao walipinga hatua hiyo wakisema kwamba hatua hiyo inawaharibia biashara.

“Usafi tunaofanya hivi sasa sio tu kwa sababu ya ziara ya Papa,” akasema George Ya Lala, mratibu wa jiji la Kinshasa anayesimamia mchakato huo.

Alipoombwa kutoa maoni yake kuhusu kutimuliwa kwa kwa wafanyabiashara hao, mwakilishi wa kidiplomasia wa Vatican mjini Kinshasa, aliliambia shirika la habari la Reuters kupitia ujumbe mfupi wa simu kuwa usafi unaofanywa hauhusiani na ziara ya Papa.

Alisema Vatikani ilikuwa imeomba tu kwamba maandalizi ya ziara ya Papa Francis yafanywe kwa njia ya busara na bora zaidi.

“Ni wazi tunataka maeneo ya mapokezi yaweze kuwahifadhi watu wengi zaidi. Kadhalika, tunataka pia barabara ziwe salama.”

Kulingana na mfanyabiashara David Mbemba, 19, amepoteza pesa nyingi katika shughuli hiyo ya kubomolewa kwa vibanda.

Wafanyabishara wengi kama Jean Mbuyu walisema wamepoteza kila kitu kwa kuwa hawakupewa onyo wala notisi ya kuhama.

Ya Lala alipinga hilo, akisema wafanyabiashara walikuwa wamepewa notisi mapema kabla ya shughuli hiyo kuanza.

Baadhi ya wakazi wa nchi hiyo wanategemea biashara.

“Mimi ni mjane. Lazima nilipe karo…sasa nitakufa kwa sababu ya njaa,” akasema Marth Kayunga, mfanyabiashara katika soko moja kwenye mitaa iliyo kando ya Lumumba Boulevard inayolengwa na kikosi hicho kinachofanya usafi.

“Tulijua operesheni hii ilikuwa ya kusafisha Lumumba Boulevard kabla ya ziara ya Papa ambayo sote tunaisubiri,” akasema Jesus, mmiliki wa duka la vifaa vya ujenzi.

“Tunashangaa polisi wanaingia kwenye mitaa midogo kwa sababu walituambia wanaenda tu kuondoa uchafu kwenye barabara kuu. Sio haki.”

Msemaji wa polisi alisema wanatumia maagizo ya mkuu wa mkoa wa Kinshasa na mamlaka ya jiji kama vile Ya Lala, ambaye alikuwa na polisi uwanjani akiongoza operesheni hiyo.

  • Tags

You can share this post!

KCSE 2022: Arabuko Forest High yapata matokeo mazuri

Wagonjwa wakosa dawa katika hospitali ya Thika Level 5

T L