• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
Viongozi wa Chadema wakataa kikao na rais

Viongozi wa Chadema wakataa kikao na rais

Na MASHIRIKA

DODOMA, Tanzania

VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jumatano walisusia mkutano wa kujadili demokrasia ulioongozwa na Rais Samia Suluhu.

Rais Suluhu alikutana na viongozi wa upinzani kujadili suala la demokrasia nchini humo kwenye mkutano ulioandaliwa na afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa na baraza la vyama vya siasa.

Viongozi wa Chadema, ambao kiongozi wao Freeman Mbowe amekuwa kizuizini tangu Julai 2021 kwa madai ya kuhusika na ugaidi, walisusia mkutano huo wakishutumu serikali kwa kunyanyasa wanasiasa wa upinzani.

“Huo sio mkutano wa kujadili hali ya demokrasia. Ni wa kuhalalisha vita haramu dhidi ya wapinzani na ukandamizaji wa demokrasia chini ya utawala wa Magufuli na wa Samia. Bila kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa na kuruhusiwa mikutano ya hadhara sisi hatutashiriki,” akasema naibu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ambaye sasa anaishi uhamishoni nchini Ubelgiji.

Katika hotuba yake, hata hivyo, Rais Suluhu alidokeza kuwa yuko tayari kumsamehe Mbowe ambaye, kesi yake ya ugaidi inaendelea kusikilizwa kortini.

Rais alidokeza hilo baada ya kuombwa na kiongozi wa chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe, ambaye alitaka amsamehe Mbowe.

“Kama mlezi, kama mkuu wa nchi, nina jukumu na wajibu wa ulezi. Kama mlezi natakiwa kuwa mvumilivu msikivu na mwenye kusamehe na niko tayari kufanya yote haya. Nitasikiliza, nitavumilia mnayoniambia, mnayonikosoa na niko tayari kusamehe ili twende vyema. Mimi nimesimama, ninasema mbele yenu wengine wako kwenye vyombo vya habari wananiona na ulimwengu unanitizama niko tayari kuvumilia kustahamili na kusamehe,” alisema Rais Suluhu.

Lakini kiongozi huyo alishikilia kuwa Mbowe alivunja sheria.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa mkutano wa aina hii kufanyika tangu Rais Suluhu kuingia mamlakani mnamo Machi 2021 kufuatia kifo cha John Pombe Magufuli.

Rais Suluhu aliwataka wanaoshiriki mkutano huo kujadili mbinu bora ya kufanya mikutano ya hadhara bila kuvuruga amani na kutukanana.

Kauli hiyo ya Rais inaonekana kuleta matumaini mapya kwa vyama vya kisiasa baada ya mikutano ya hadhara kupigwa marufuku.

Tayari serikali imefutilia mbali kesi zote zilizokuwa zikimwandama Lissu, ambaye alitorokea Ubelgiji baada ya kudai kuibiwa kura za urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2020, ambapo hayati Magufuli aliibuka mshindi kwa zaidi ya asilimia 80 ya kura.

Lissu, ambaye 2017 alinusurika kifo baada ya kushambuliwa kwa bunduki jijini Dodoma, hata hivyo, alisema hachukulii kufutwa kwa kesi hizo kama hakikisho la usalama wake.

You can share this post!

JUMA NAMLOLA: Serikali iboreshe uchukuzi wa umma kuokoa...

Akiri kuiba simu KNH na kutorokea mochari

T L