• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Akiri kuiba simu KNH na kutorokea mochari

Akiri kuiba simu KNH na kutorokea mochari

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMUME aliyeiba simu na kutorokea ndani ya mochari kujinusuru alishtakiwa Ijumaa.

Abdikadir Idris aliyekiri shtaka la kuiba simu katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) Desemba 4, 2021 alimweleza hakimu mkuu Bi Susan Shitubi kwamba “ilibidi nitorokee mochari niponye maisha yangu ili nisiuawe na umati wa watu.”

Idris alisababisha kicheko aliposema, “Ningalizubaa hata mimi ningalilazwa mochari. Ilibidi nichomoke mbio. Ilikuwa ni mguu niponye.”

Aliposomewa mashtaka mawili ya wizi na kupatikana na mali ya wizi mnamo Desemba 4, 2021 KNH, Idris alikiri mashtaka na kuomba msamaha akisema amejutia matendo yake maovu yaliyomfanya aingie mochari akiwa hai.

“Nilijua hakuna mtu aliye na ukakamavu wa kunifuata ndani ya mochari,” mshtakiwa huyo alieleza hakimu.

Mshtakiwa huyo alikamatwa na mabawabu wanaolinda mochari ya KNH na kukabidhiwa maafisa wa polisi.

Kiongozi wa mashtaka alieleza mahakama kwamba Idris aliiba simu hiyo kutoka kwa mwendesha pikipiki ya kazi ya bodaboda Simon Wekesa Kwoba.

Thamani ya simu hiyo muundo wa Samsung A02 ni Sh17,000.

Idris alikuwa amebebwa na Kwoba kutoka Parklands kumpeleka KNH kununua dawa ya baba yake.

Mahakama ilielezwa walipofika mle mshtakiwa alimwomba mlalamishi simu apige akidai alisahau yake nyumbani.

Kwoba alimsaidia mshtakiwa ambaye alienda hatua chache azungumze akitumia simu lakini akachomoka mbio.

Mshtakiwa alitorokea mochari ya KNH huku amefuatwa unyounyo.

Mabawabu walimwokoa kwa kumkamata asipate ghadhabu ya wananchi.

Mabawabu walimpokonya simu mshtakiwa kisha wakamkabidhi mikononi mwa polisi.

Simu hiyo ilitolewa mahakamani kama ushahidi tosha.

Mshtakiwa alizuiliwa kwa wiki mbili ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia iwasilishwe kortini.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wa Chadema wakataa kikao na rais

Lewandowski avunja rekodi nyingine ya ufungaji mabao...

T L