• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
Wanawake wanaovaa vimini na suruali za kuonyesha shepu ya makalio kutozwa faini Sh3,000

Wanawake wanaovaa vimini na suruali za kuonyesha shepu ya makalio kutozwa faini Sh3,000

NA JANETH MUSHI, MWANANCHI

ARUSHA, TANZANIA

KUTOKANA na kuporomoka kwa maadili hasa kwa vijana katika maeneo mengi nchini Tanzania, uongozi wa kijiji cha Olevolosi, kata ya Kimnyaki wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha umeweka sheria ndogo mbalimbali na kupitishwa na mkutano mkuu wa kijiji.

Miongoni mwa yaliyopitishwa ni pamoja na kupiga marufuku wasichana au wanawake kuvaa suruali za kubana au sketi fupi ‘vimini’, kijana wa kiume kusuka nywele au kunyoa pembezoni mwa kichwa na kuacha nywele katikati ‘kiduku’, kuvaa hereni au kuvaa suruali inayoonyesha makalio na adhabu za makosa hayo ni faini Sh50,000 (sawa na Sh3,000 za Kenya).

Akizungumza katika mkutano mkuu wa kijiji hicho, Mtendaji wa Kata hiyo ya Kimnyak, Joshua Mollel, aliwasilisha sheria hizo kwa niaba ya mtendaji wa kijiji hicho, ambazo zilipitishwa na mkutano huo.

“Marufuku kwa msichana au mwanamke yoyote kuvaa suruali ya kubana na kuonyesha maungo yake au kimini ukibainika faini yake ni Sh50,000 na kama hauna hapo kuna akina mama walioandaliwa tumeambiwa tuwaletee,” amesema.

“Marufuku kwa kijana yoyote wa kiume kusuka nywele au kunyoa pembezoni mwa kichwa,na kuacha katikati ‘kiduku’ au kuvaa suruali mlegezo inayoonyesha makalio au kuvaa suruali iliyotobolewa, faini yake ni Sh50,000 na kama huyo kijana hana kuna adhabu nyingine wazee wamependekeza,” amesema mtendaji huyo.

Sheria nyingine ni kupiga marufuku kijana wa kiume kuvalia hereni, marufuku kijana mwenye nguvu kutokufanya kazi na atakayeonekana kijiweni asubuhi bila kufanya kazi atatozwa faini Sh50,000, ni kosa kupika au kuuza pombe haramu ya gongo na adhabu yake ni kupelekwa mahakamani na atakayekutwa na anauza pombe muda wa kazi atatoza faini Sh50,000.

Baada ya kusoma mapendekezo hayo ya sheria ndogo hizo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Olevolosi, Emanuel Ngauliva aliuliza wananchi hao walioshiriki kikao hicho endapo wanapitisha sheria hizo, ambapo wananchi hao waliridhia na kuzipitisha kama sheria ndogo.

“Imepita kwa kishindo kuanzia leo (jana Jumatatu) ukikamatwa na makosa hayo utapewa akaunti namba utaenda kuweka fedha hizo na kuna kamati husika itafanya hiyo kazi. Kama kuna aliyevaa suruali hapa tuanze kufanya naye kazi hapa kama kuna kijana amenyoa kiduku au amevaa hereni tufanyie kazi hapa na tutakuwa na sungusungu wanapita katika vitongoji kukagua,” amesema.

Mmoja wa wananchi hao, Olariv Robert amesema yeye ni miongoni mwa walioshirikiana na viongozi kuunda sheria hizo ndogo kufuatilia matukio yaliyotokea kijijini hapo ya vijana waliouawa kwa kudaiwa kuiba na kuwa waliona hilo limesababishwa na maadili kuporomoka.

“Uongozi wa kijiji na wazee wa ukoo wakakubalia sheria ndogondogo zitumike na sisi kama wananchi tumekutana kupitisha jamii irudi katika mstari wa mbele,” amesema.

Naye Lily Lazaro amesema wanaamini sheria hizo zinasaidia kubadili maadili kwa jamii hasa watoto.

Aidha kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt Dorothy Gwajima imepongeza jitihada za kijiji hicho kutunga sheria ndogo hizo zitakazowaongoza kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.

Amesema kuwa changamoto ya mmomonyoko wa maadili imezidi kuchukua sura mpya kila siko katika jamii, huku Serikali kwa kushirikiana na wadau ikifanya jitihada mbalimbali kukabiliana na hali hiyo ikiwemo programu zinaziratibiwa na wizara hiyo za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa lengo la kuhakikisha wanakuwa katika misingi bora ya maadili mema.

“Hatua hiyo ni kubwa kwa jamii yetu kuamua yenyewe kutunga sheria zao kuhusu maadili, kwani kila wakati mmekua mkitoa wito kwa viongozi hasa wa mamlaka za serikali za mitaa kubeba ajenda ya kusaidia jamii kwenda mbele hasa katika maadili, fursa za kiuchumi na kupinga ukatili,” imesema taarifa hiyo.

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Uhaba wa dawa za TB wahatarisha afya ya...

Pasta ‘fisi’ alia akilaumu muumini kwa...

T L