• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
SHINA LA UHAI: Uhaba wa dawa za TB wahatarisha afya ya Wakenya

SHINA LA UHAI: Uhaba wa dawa za TB wahatarisha afya ya Wakenya

NA PAULINE ONGAJI

AGOSTI 2023, Bw Emanuel Parsare, mkazi wa kijiji cha Kiserian, eneo la Marigat, Kaunti ya Baringo, alizuru hospitali ya kaunti ndogo ya Marigat, ili kupimwa kikohozi kubaini ikiwa alikuwa na maradhi ya kifua kikuu (TB).

Hata hivyo, asema kwamba baada ya kusubiri matokeo hayo ambayo yalikuwa yanachukua muda, aliamua kuenda katika hospitali ya kibinafsi eneo hilo na kupigwa picha za eksirei, ambazo zilithibitisha kwamba alikuwa na maradhi ya TB.

“Baada ya hapo, nilipeleka matokeo hayo katika hospitali ya kaunti ndogo ya Marigat ambapo uchunguzi zaidi wa maabara ulifanywa na ukathibitisha kwamba nilikuwa nauugua.”

Kwa hivyo, Bw Parsare asema, alianza matibabu mara moja.

“Nilipewa dawa kadhaa zilizotarajiwa kukamilika baada ya wiki mbili, ambapo baadaye ningehitajika kurejea hospitalini kupewa nyingine,” aeleza.

Muda huo uliisha siku ya Jumamosi, Septemba 30, 2023, lakini hata kabla ya siku hiyo kutimu, Bw Parsare asema kwamba tayari kulikuwa na baadhi ya dawa alizokuwa amepewa ambazo zilikuwa zimekwisha.

“Nina wasiwasi kwa sababu kwa siku hizo chache ambazo sijatumia dawa hizo zilizokwisha, kikohozi ambacho kilikuwa kinatokomea, kimeanza kurejea.”

Japo kumekuwa na taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba baadhi ya sehemu zilizoathirika zilipokea dawa, kufikia jana Jumatatu Bw Parsare hakuwa amepata dawa.

“Naishi mbali ambapo usafiri kutoka kijijini hadi hospitalini unachukua saa mbili kwa gari, na siwezi toka tu kwenda bila kuulizia. Aidha, nauli ya kwenda huko kila mara na kukosa dawa ni ghali,” aeleza.

Wagonjwa wengi

Hii ndio taswira inayokumba wagonjwa wengi wa TB katika eneo hili. Kulingana na mhudumu mmoja wa kijamii wa afya eneo hilo, tangu mwisho wa mwezi wa Agosti, wamekumbwa na uhaba wa aina kadhaa za dawa za TB.

“Mambo ni mabaya sana kiasi cha kwamba kuna wagonjwa saba hapa ambao hawajaanza kutumia dawa licha ya kugundulika kuwa na maradhi haya.”

Bw Stephen Shikoli, mratibu wa kitaifa wa muungano wa wanaharakati wa kukabiliana na ugonjwa wa TB anathibitisha kwamba kwa kweli kuna uhaba wa dawa za kutibu maradhi haya nchini.

Mwanaharakati mwingine ambaye hakutaka kutajwa anasema kwamba baadhi ya wagonjwa hawapati dawa kabisa, na kwa wale wanaopata, inabidi wapewe kwa vipimo.

“Kunao ambao hata hawajaanza kutumia dawa kwani wahudumu wa afya wanamakinika na kushughulikia wale ambao tayari wameanza matibabu. Tumelazimika kuagiza dawa kutoka mataifa jirani ya Uganda.”

Kulingana na Bw Shikoli, mpango wa kitaifa unaoshughulikia maradhi ya TB, NLTP, umekuwa ukisambaza pakiti chache za dawa hizi kwa kaunti.

“Kuna baadhi ya wagonjwa wanaolazimika kutumia pakiti za dawa za TB kwa pamoja, huku wengine wakiwa hawajaanza matibabu,” aongeza.

Kwa kawaida, mgonjwa wa TB anapoanza matibabu yeye hupewa pakiti kamili ya dawa ambazo zinapaswa kukamilisha matibabu ya miezi sita. Pakiti hizi huhifadhiwa hosptalini ili mgonjwa anapokuja anapokea dawa za wiki mbili kwa dozi ya mwezi mmoja.

Wagonjwa ambao wameanza kupata nafuu huja kliniki kila baada ya wiki mbili kujaza dawa na kufanyiwa ukaguzi wa kimatibabu katika awamu ya kwanza ya matibabu ambayo ni miezi miwili.

Baada ya hapa, sasa mgonjwa atahitajika kuja hospitalini mara moja kwa mwezi katika kipindi cha miezi hiyo minne iliyosalia.

“Lakini kwa sasa, kutokana na uhaba huu, sasa wagonjwa wanaweza kupewa dawa za pengine siku tano, kumaanisha kwamba basi uwezekano wa wagonjwa hao kutorejea hospitalini uko juu hasa ikizingatiwa kwamba idadi kubwa ya wagonjwa wanafanya kazi za sulubu kumaanisha kwamba wasipoenda kazini basi hawalipwi,” aongeza Bw Shikoli.

Ruhusa kazini

Aidha, Bw Shikoli asema kwamba kuna baadhi ya wagonjwa ambao wamelazimika kuomba ruhusa kazini mara kadhaa kuja hospitalini kupokea dawa, lakini kila wanapokuja wanakosa dawa, suala linalowaweka katika hatari ya kupoteza ajira.

Katika sehemu nyingine, asema, hata kuna wanafunzi ambao wamelazimika kutoenda shule kwa siku kadhaa, kwa sababu imewalazimu kuomba ruhusa na kuja hospitalini mara kwa mara kubahatisha ikiwa watapata dawa.

“Pia, hii inaathiri familia kwani ikiwa mhusika atalazimika kumuomaba mwenzake ruhusa kila mara kwenda hospitalini, basi huenda ikaonekana kana kwamba anadanganya.”

Lakini kando na masuala ya kijamii, kuna hatari kubwa ya kiafya inayokodolea sio tu wagonjwa walioathirika, bali pia kwa jamii na nchi kwa jumla.

Daktari mmoja mtaalam wa maradhi haya ambaye hakutaka kutajwa asema kwa wagonjwa ambao wameanza kutumia dawa kisha wakasitisha, kuna hatari ya maradhi haya kubadilika na kuwa sugu, suala linaloongeza gharama ya matibabu.

Ripoti iliyotolewa na Wizara ya Afya miaka miwili iliyopita ilionyesha kwamba gharama ya kuwatibu wagonjwa wanaougua TB sugu ni mara sita zaidi ya ile ya kutibu TB ya kawaida.

Kulingana na daktari huyo, wagonjwa wanaozidi kutangamana na jamii pasipo kupokea maradhi haya, ni hatari kwani kuna uwezekano mkubwa wa wao kusambaza zaidi ugonjwa huu, na hivyo kuongeza mzigo wa TB nchini.

Kulingana na maktaba ya matibabu ya mgonjwa wa TB hugharimu serikali zaidi ya Sh25,000. Huu ni mzigo mkubwa zaidi wa kiuchumi kwa mfumo wa afya nchini.

Mataifa jirani

Kumbuka kwamba tayari Kenya ni miongoni mwa mataifa yaliyoathirika pakubwa na maradhi ya TB. Nchi hii imeorodheshwa miongoni mwa mataifa 30 yanayochangia zaidi ya asilimia 80 ya visa vya TB.

Kulingana na duru kutoka kwa mpango wa NLTP, kwa kweli kuna uhaba wa dawa japo sio tatizo linaloathiri Kenya pekee.

“Uhaba huu unashuhudiwa hata nchini India, na katika baadhi ya mataifa jirani ambapo tumekuwa tunanjaribu kusuluhisha shida hii,” alisema afisa huyo ambaye hakutaka kutajwa.

Lakini Bw Shikoli asema kwamba tatizo ni kwamba hakujakuwa na taarifa rasmi kutoka kwa vitengo husika kuhusiana na hali halisi ya mambo yalivyo nchini.

Haya yakijiri, wagonjwa wa TB nchini wanaendelea kuumia huku raia wengine wakiwa katika hatari ya kuambukizwa maradhi haya.

  • Tags

You can share this post!

Karen Nyamu: Harusi nyingine ya Akothee ikifanyika...

Wanawake wanaovaa vimini na suruali za kuonyesha shepu ya...

T L