• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 4:32 PM
Wanawake washtumiwa kwa kushiriki fujo wakati wa siku ya kimataifa

Wanawake washtumiwa kwa kushiriki fujo wakati wa siku ya kimataifa

NA FARHIYA HUSSEIN

MASHIRIKA yamelaani vikali fujo zilizoshuhudiwa Jumanne wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake jijini Mombasa.

Katika kisa hicho uwanjani Tononoka, baadhi ya wanawake wanaotofautiana kisiasa, walishambuliana kwa makonde, huku kukiwa pia na wanaume walioungana nao.

Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Haki Africa lilitaja tukio hilo kuwa la aibu hasa wakati ambapo wanawake wengine wanajitahidi kujitenga na fujo za kisiasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwa Uchaguzi Mkuu.

“Tuachane na tabia hizi mbovu na badala yake tulenge macho yetu kwa maendeleo ya wanawake. Tunatoa wito pia kwa asasi za kiusalama kuchukulia hatua waliopanga fujo hizo,” akasema Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Bi Salma Hemed.

Siasa

Wakati huo huo, kikundi kipya cha wanawake kimetangaza mipango ya kusimamisha wagombeaji ugavana wa kike katika kila kaunti ya Pwani.

Hayo yamejiri huku wanawake katika maeneo ya Pwani, wakihimizwa kuwa na ari ya kuwania viti tofauti vya kisiasa na wala si wadhifa wa mbunge mwakilishi wa kike pekee.

Wito huo ulitolewa wakati viongozi wa kike kutoka eneo hilo, walipozindua kundi la ‘Pwani Women Caucus Group’ linalolenga kuhamasisha wanawake zaidi kuwania viti vya kisiasa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti.

Bi Hemed, alisema lengo kuu la kundi hilo ni kuhakikisha kuwa watasimamisha mwanamke mmoja kuwania kiti cha ugavana katika kila kaunti ya Pwani.

“Tunataka kukomesha dhana kwamba wanawake wanatumika kwa urahisi katika mashindano ya uchaguzi. Tunataka kuhakikisha sisi, wanawake tunakuwa katika nyadhifa za juu za kisiasa katika ukanda wa Pwani,” alisema Bi Hemed.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na wanawake wengine wanaotaka kuwania viti tofauti vya kisiasa katika uchaguzi ujao, ambao walieleza ajenda wanazonuia kutimiza endapo watachaguliwa mamlakani.

“Wanawake hawapaswi kugombea nafasi moja tu ya kisiasa. Nafasi ya Mbunge Mwakilishi wa Kike ni kiti cha usaidizi kinachosaidia kuwainua wanasiasa wa kike kuwania viti vingine vya juu. Sote tujikakamue,” akasema Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko.

Mwezi Februari, wagombea wa kike Pwani, walimtaka Mkuu wa polisi wa Pwani kupanga mkutano nao ili kujadili masuala yao ya usalama.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Wakenya wangali wamegawanyika licha ya...

Bayern waingia robo-fainali za UEFA baada ya kurarua RB...

T L