• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Bayern waingia robo-fainali za UEFA baada ya kurarua RB Salzburg bila huruma

Bayern waingia robo-fainali za UEFA baada ya kurarua RB Salzburg bila huruma

Na MASHIRIKA

ROBERT Lewandowski alifunga mabao matatu chini ya dakika 23 za kipindi cha kwanza katika ushindi wa 7-1 uliosajiliwa na Bayern Munich dhidi ya RB Salzburg ya Austria kwenye mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne usiku ugani Allianz Arena.

Mechi hiyo ilikuwa ya 100 kwa Lewandowski kusakata katika soka ya UEFA. Fowadi huyo ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Poland alifungulia Bayern ukurasa wa mabao kupitia penalti mbili chini ya dakika 21 za kwanza baada ya kuchezewa visivyo na beki wa Salzburg, Maximilian Wober.

Bao la kwanza la Lewandowski lilikuwa lake la 40 kufikia sasa katika mashindano yote msimu huu. Alipachika wavuni goli lake la tatu dhidi ya Salzburg katika dakika ya 23 baada ya kumwacha hoi kipa Philipp Kohn.

Ni mara ya pili katika historia ya UEFA kwa mabao matatu katika mchuano mmoja kufungwa na mchezaji mmoja chini ya dakika 23. Bafetimbi Gomis aliwahi kupachika wavuni mabao matatu chini ya dakika nane katika ushindi wa 7-1 uliosajiliwa na waliokuwa waajiri wake Olympique Lyon dhidi ya Dinamo Zagreb mnamo 2011. Nyota huyo raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 36 sasa anachezea Galatasaray ya Uturuki.

Bayern walishuka dimbani dhidi ya Salzburg wakiwa na ulazima wa kushinda baada ya miamba hao wa Austria kuwalazimishi sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza mnamo Februari 16, 2022.

Chini ya kocha Matthias Jaissle, Salzburg walipoteza nafasi nyingi za wazi kupitia Nicolas Capaldo na Nicolas Seiwald.

Mabao mengine ya Bayern ambao sasa wamefuzu kwa robo-fainali kwa jumla ya mabao 8-2, yalifumwa wavuni kupitia Serge Gnabry, Thomas Muller na Leroy Sane.

Salzburg walijibwaga ulingoni wakilenga kuwa kikosi cha cha Ligi Kuu ya Austria kuwahi kuingia robo-fainali za UEFA tangu 1985.

Lewandoski sasa anajivunia mabao 85 katika historia ya UEFA, matatu chini ya Lionel Messi wa PSG na 17 zaidi nyuma ya Cristiano Ronaldo wa Manchester United.

Baada ya Ronaldo na Messi, Lewandowski sasa ndiye mchezaji mwingine kuwahi kufunga zaidi ya mabao 10 katika zaidi ya misimu mitatu mfululizo ya UEFA.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wanawake washtumiwa kwa kushiriki fujo wakati wa siku ya...

Ruto aonekana kuwa kigeugeu akiwa ng’ambo

T L