• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:26 PM
Watu 600,000 wameuawa katika vita Tigray – Obasanjo

Watu 600,000 wameuawa katika vita Tigray – Obasanjo

NA MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KIONGOZI wa juhudi za upatanisho kwenye mzozo ambao umekuwa ukiendelea katika eneo la Tigray nchini Ethiopia, Olusegun Obasanjo, amesema kuwa hadi watu 600,000 wamefariki kutokana na mapigano hayo.

Mapigano hayo yalianza mwishoni mwa mwaka wa 2020 kati ya jeshi la Ethiopia na wanamgambo wa Tigray People’s Liberation Front (TPLF) katika eneo la kaskazini.

Obasanjo, ambaye ni rais wa zamani wa Nigeria, alisema hayo kwenye mahojiano na jarida la Financial Times.

“Kuna uwezekano idadi ya waliofariki ni 600,000,” akasema.

Alisema kuwa wakati wa kutiwa saini kwa mkataba wa amani baina ya pande hizo mbili nchini Afrika Kusini, Novemba 2022, maafisa kutoka Ethiopia walieleza furaha yao kwa kusitisha mapigano hayo yaliyokuwa yakisababisha “vifo vya karibu watu 1,000 kila siku”.

Mapigano hayo yalizuka Novemba 2020 baada ya wanamgambo wa TPLF kushambulia kambi kuu ya kijeshi katika eneo la Mekelle.

Kufuatia shambulio hilo, Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliagiza operesheni kali dhidi ya kundi hilo.

Hilo pia lilichangiwa na taharuki kali ya kisiasa iliyokuwepo baina baina ya pande hizo mbili.

TPLF ilikuwa imekataa kutambua uamuzi wa serikali ya Ethiopia kufutilia mbali tarehe ya kuandaa uchaguzi mkuu na kuandaa chaguzi za kimaeneo nje ya jiji la Addis Ababa.

TPLF imekuwa ikimlaumu Abiy kwa kuongeza taharuki za kisiasa katika nchi hiyo tangu alipochukua uongozi mnamo Aprili 2018.

Ndiye mtu wa kwanza kutoka kwa jamii ya Waoromo kuhudumu kama Waziri Mkuu.

Hadi 2018, kundi la TPLF ndilo lililokuwa likidhibiti siasa za taifa hilo tangu 1991.

Wanamgambo hao walikuwa wakiunga mkono chama kingine kikubwa—Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF).

Chama hicho kilikuwa kikipinga juhudi za mageuzi ambazo zimekuwa zikiendelezwa na Abiy.

Wadadisi na mashirika ya kimataifa yanasema kuwa huenda takwimu zilizotolewa na Obasanjo zikawa za kweli.

Mtafiti Tim Vanden Bempt kutoka Chuo Kikuu cha Ghent, nchini Ubelgiji, anasema idadi ya watu ambao wameuawa kwenye mapigano hayo ni kati ya 300,00 na 400,000 kutokana na mashambulio ya kivita, njaa na ukosefu wa huduma bora za afya.

Mtafiti huyo anakubaliana na tathmini kadhaa ambazo zinasema kuwa kuna uwezekano kuna kati ya watu 200,000 na 300,000 ambao hawajajumuishwa.

Hata hivyo, baadhi ya maafisa wa serikali ya Ethiopia ambao hawakutaka kutajwa walisema kuwa takwimu hizo “zimetiwa chumvi”. Wanakisia idadi ya watu waliouawa ni kati ya 80,000 na 100,000.

Kiongozi wa Tume ya Kutetea Haki za Binadamu ya Ethiopia (EHRC), Daniel Bekele, aliomba uwepo wa tahadhari kuhusu suala hilo.

“Huenda tukakosa kujua idadi kamili ya watu waliofariki kwenye mzozo huu. Lazima tuwe waangalifu tunapotoa takwimu hizo kwani huenda baadhi zimeongezwa chumvi kupita kiasi,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Hisia mseto polisi sasa wakinyoa wenye rasta

SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa matumbwitumbwi unavyoathiri watu...

T L