• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa matumbwitumbwi unavyoathiri watu wazima

SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa matumbwitumbwi unavyoathiri watu wazima

NA WANGU KANURI

MNAMO Desemba 2022, Chrismus Kimaru, 39, mkazi wa Ruai, Kaunti ya Nairobi, alianza kulalamika akielezea kuhisi uchovu, tezi za mate kumvimba, maumivu kwenye moja ya korodani zake huku ikimtatiza kutoka kitandani.

Kama hulka ya Wakenya haswa wanapojihisi kuwa hali yao ya afya si shwari, Bw Kimaru alifanya uchunguzi wake mtandaoni kulingana na dalili alizokuwa nazo, na kupata kuwa alikuwa akiugua ugonjwa wa matumbwitumbwi (mumps).

Wazo la kupekua mtandao na kuchunguza ugonjwa uliokuwa ukimtatiza lilimjia Bw Kimaru haswa sababu mwanawe alikuwa na ugonjwa huo mwanzoni mwa Novemba.

Hata hivyo, alifanya shughuli zake za kila siku licha ya maumivu yale lakini akalemewa kula chamcha vizuri pamoja na kuhisi kana kwamba alikuwa akipata homa.

Jioni, akielekea nyumbani, Bw Kimaru alitembea kwa uchungu.

“Usiku huo, kichwa kilimuuma sana na akawa akihisi joto jingi mwilini na kutiririkwa na jasho. Kitanda kilikuwa kama kimemwagiwa maji,” anasimulia.

Zaidi ya korodani kuwa na maumivu, ilikuwa imefura. Vyakula vyenye chachu vikawa vikimtatiza kula.

“Nilienda kwenye duka la dawa na kupata dawa za kupunguza maumivu niliyokuwa nayo lakini hazikunifaa. Maumivu yalipozidi, nilienda kwenye kliniki moja karibu na ninakoishi ili kupata ushauri zaidi,” anaeleza.

Wakati huu, alikuwa akivaa barakoa ili kuficha tezi zake zilizokuwa zimefura. Alibadilishiwa dawa alizokuwa amepewa awali na kushauriwa apumzike huku daktari akimweleza kuwa alikuwa akiugua ugonjwa wa mumps.

Dkt Victor Ng’ani mtaalamu wa ugonjwa wa mumps.

Vile vile daktari huyo alimshauri dhidi ya kutangamana na watu ili kuzuia uenezi na uambukizanaji.

Ugonjwa wa mumps husababishwa na virusi huku ukiathiri tezi za mate. Kwa watu wengi, ugonjwa huo huzifanya tezi hizo ambazo huwa kwenye uso, sehemu ya chini ya sikio kuvimba na kuonekana kwenye ufizi.

Safari ya kutibu mumps kwa Bw Kimaru ilikuwa ndefu huku akikata tamaa kwa kuhisi kama dawa hazimsaidii. Anaeleza kuwa nyakati zingine alihisi joto jingi huku wakati mwingine baridi jingi.

Hata hivyo, katika hali hilo alilazimika kutafuta ushauri wa daktari mwingine ambaye alimhakikishia kuwa hali yake ya afya itaimarika iwapo ataendelea kumeza tembe alizopewa.

“Daktari huyo alinieleza kuwa kuna uwezekano nilipata mumps kutoka kwa mwanangu licha ya kuwa alikuwa ashapata afueni,” anasema.

Vile vile, alishauriwa kutembea mara kwa mara na kumaliza dawa alizokuwa nazo. Hata hivyo, kwa kuwa ugonjwa huo huathiri watoto zaidi, watu wengi hawakuelewa mbona aliupata akiwa mtu mzima.

Dkt Victor Ng’ani, mtaalamu katika hospitali ya RFH Healthcare, anasema kuwa ugonjwa huo huathiri sehemu nyingi za mwili.

Dalili zake ni pamoja na kuhisi joto jingi mwilini, uchovu, kufura kwa ufizi pamoja na viungo mwilini, maumivu ya kichwa, kutokuwa na hamu ya kula, kushindwa kutafuna chakula pamoja na kupata homa.

“Zaidi ya hayo, ugonjwa wa mumps humfanya mtu kupoteza uwezo wa kusikia, kufura kwa utando unaofunika akili na uti wa mgongo pamoja na kongosho. Kwa wanaume, korodani moja au zote hufura huku matiti ya mwanamke pamoja na ovari zake hufura aidha moja au zote mbili,” anasema Dkt Ng’ani.

Asilimia 20 ya wanaume waliougua mumps hulalamikia maumivu ya korodani, uwezo wao wa kuzalisha unaweza ukapunguka kwa muda lakini si milele.

Vile vile, kunao uwezekano wa mimba kuharibika kwa mwanamke mwenye ujauzito wa wiki 12 anayeugua mumps.

Hata hivyo, Dkt Ng’ani anaeleza kuwa licha ya kutokuwepo kwa dawa mahususi ya kutibu mumps, madaktari huwatibu wagonjwa wao kwa kudhibiti dalili.

“Ni vyema kwa mgonjwa wa mumps kupumzika nyumbani kwa siku kadhaa ili kupunguza uenezaji. Pia anapaswa kuhakikisha kuwa ananawa mikono vizuri, anafunika mdomo anapopiga chafya au kukohoa na anasafisha maeneo anayoshika sana kama mojawapo ya njia za kudhibiti ugonjwa huo.”

Huku Bw Kimaru akiwa miongoni mwa watu walioathiriwa na ugonjwa huo haswa katika kaunti ya Nairobi mwezi Desemba 2022, Kituo cha Kudhibiti Maradhi (CDC), kinasema kuwa ugonjwa huo huenea iwapo mtu mwenye virusi hivyo atatangamana na mtu asiyekuwa navyo.“Utapata mumps iwapo utatumia chupa moja ya maji na mtu anayeugua mumps, kupigana busu, kucheza au kushirikiana kwa njia yoyote ile,” CDC inaeleza.Dalili za mumps huanza kujitokeza siku 12 hadi 25 baada ya kupata maambukizi huku watu wengine wakikosa kupata dalili hata moja. Wagonjwa wengi wa mumps hupata afueni baada ya wiki mbili.Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa wagonjwa wa mumps huweza kuambukiza watu wengine siku mbili hadi tisa kabla ya tezi za mate kufura.“Mumps hutokea wakati wowote kwenye maeneo yenye joto jingi, baridi nyingi au nyakati ambazo hamna jua au baridi nyingi. Nchi nyingi huripoti mkurupuko kila baada ya miaka miwili hadi mitano,” ripoti ya WHO inasema.

Dkt Victor Ng’ani, mtaalamu katika hospitali ya RFH Healthcare, anasema kuwa ugonjwa wa mumps huathiri sehemu nyingi za mwili. PIC

  • Tags

You can share this post!

Watu 600,000 wameuawa katika vita Tigray – Obasanjo

MAPISHI KIWETU: Firigisi ya kuku

T L