• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Waziri ajiuzulu kufumaniwa akibusiana na msaidizi wake

Waziri ajiuzulu kufumaniwa akibusiana na msaidizi wake

Na AFP

LONDON, Uingereza

WAZIRI wa Afya wa Uingereza Matt Hancock ambaye ameongoza taifa hilo katika vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, alijiuzulu wikendi baada ya kunaswa kwenye kamera akimpiga busu mmoja wa wasaidizi wake ambaye anadaiwa kuwa ni mpenzi wake.

Hancock alisema alichukua hatua hiyo kama kielelezo bora, akikiri kwamba hakuongoza kwa mfano, kwa kukiuka wazi sheria za kupambana na virusi vya corona.

Mnamo Ijumaa, Hancock aliomba msamaha kwa kukiuka masharti ya kuzuia corona kwa kumpiga busu Gina Coladangelo mnamo Mei 6.

Wakati huo sheria za corona bado hazikuwa zimelegezwa na ilikuwa marufuku kupigana pambaja au kupigana busu kutokana na hatari ya kuambukizwa corona.

Hancock alisema kuwa wengi wa raia wa Uingereza walionyesha uzalendo kwa kufuata masharti hayo kikamilifu ilhali yeye aliyakiuka, kwa hivyo, hakuwa na budi kujiuzulu hata baada ya kuomba msamaha mnamo Ijumaa.

“Mimi ni sehemu ya uongozi ambao ulitengeneza sheria hizi za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona. Lazima niongoze kwa mfano na kufuata sheria hizi kikamilifu. Hii ndiyo maana nimejiuzulu baada ya kuzikiuka hadharani,” akaandika kwenye barua yake ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Boris Johnson.

Nafasi ya Hancock itachukuliwa na Sajid Javid ambaye hapo awali alisimamia kitengo cha Hazina ya Kitaifa ya Kifedha kabla ya kujiuzulu mnamo Februari 2020.

Javid pia alihudumu kama Waziri wa Masuala ya nyumbani katika serikali ya aliyekuwa Waziri Mkuu Theresa May.

Johnson ambaye alikuwa amepuuza wito wa kumfuta Hancock, alimshukuru kwa huduma zake, akisema alikuwa mchapakazi hata kabla ya ujio wa virusi vya corona.

“Unapoondoka afisini, kazi uliyoifanya katika vita dhidi ya corona inaonekana wazi. Nakusifia kwa hilo na nakutakia heri,” akasema Johnson.

Msemaji wa wizara ya afya kwa chama cha upinzani cha Labour Jonathan Ashworth alimkashifu Johnson kwa kutomfuta kazi Hancock na kusubiri hadi akajiuzulu mwenyewe.

“Sitaki maisha yangu yachochee mjadala. Naomba familia yangu msamaha kwa kuwaweka katika hali hii ya mafadhaiko. Nahitaji kuwa na watoto wangu na nawaomba radhi wote baada ya tukio hilo lililonivunjia heshima,” akaongeza Hancock ambaye ana mke mmoja.

Pia serikali inakabiliwa na swali gumu kwa nini Hancock mwenye umri wa miaka 40, alimteua mpenzi wake wa pembeni ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu kuhudumu katika idara ya afya.

Kando na hayo Waziri huyo alidaiwa kuvunja kanuni za kutoa zabuni ya kununua vifaa vya kupambana na corona. Anadaiwa kuwa alitoa kandarasi hizo kwa marafikize na kushiriki ufisadi mkubwa.

You can share this post!

Chai: Bomet yapata soko Iran

Serikali yafanya ukaguzi wa shule Nakuru