• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 11:19 AM
Serikali yafanya ukaguzi wa shule Nakuru

Serikali yafanya ukaguzi wa shule Nakuru

Na RICHARD MAOSI

KATIBU wa kudumu katika Wizara ya Elimu anayeweka zingatio kwa elimu ya msingi Dkt Julius Jwan, Jumatatu ameongoza shughuli ya kukagua shule zilizoko Nakuru na Naivasha.

Ziara yake inakuja wakati ambapo wanafunzi waliofanya mitihani ya kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) wanajiandaa kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Jwan ametangamana na wanafunzi madarasani mwao, na hatimaye kuzuru mabweni pamoja na vyoo ili kuhakikisha miundomsingi iko katika hali nzuri kufanikisha masomo.

Isitoshe ameweka wazi mradi wa Elimu Sponsorship, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu kwa kuwapunguzia wazazi mzigo wa kulipa karo.

“Ni mradi ambao utasaidia wanafunzi wengi kutoka shule za umma kupata fursa ya kujiendeleza kielimu bila matatizo,” amesema.

Isitoshe amemiminia sifa Wakfu wa Equity kwa kutoa msaada kupitia Wings to Fly kwa watoto wanaotokea kwenye familia maskini humu nchini. Maeneo ya Nakuru Mashariki na Magharibi yalipata waliofaidika.

Alisema Wizara ya Elimu inafantya juhudi zote jinsi iwezekanavyo ili mwanafunzi yeyote asikose nafasi ya kujiunga na shule ya upili.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Jwan aliandamana na wasimamizi katika wizara ambapo alitembelea shule ya Moi Primary.

Wakati wa shughuli hiyo, ameridhika namna shule ya Moi ilikuwa imezingatia kiwango cha usafi,

“Licha ya janga la Covid-19 humu nchini, kila mmoja anajua kuwa watoto wetu wamekuwa na bahati sana kwa sababu walimu wakuu wameweka mikakati ya kujikinga,” akasema.

You can share this post!

Waziri ajiuzulu kufumaniwa akibusiana na msaidizi wake

Changamoto za kiufundi zachelewesha mpango wa kadi za...