• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Ahadi ya Ruto kukomesha utekaji nyara yageuka hewa kesi zaidi zikiripotiwa

Ahadi ya Ruto kukomesha utekaji nyara yageuka hewa kesi zaidi zikiripotiwa

NA FARHIYA HUSSEIN

AHADI ya Rais William Ruto kumaliza tatizo la kupotezwa kwa njia tatanishi iliibuka kama hakikisho kuu wakati alipokuwa anachukua madaraka.

Hata hivyo, kuibuka upya kwa matukio ya kutoweka kwa watu nchini ndani ya mwaka mmoja baada ya Rais Ruto kuingia ofisini kumetia shaka dhamira ya utawala wake katika kulinda haki za binadamu.

Wakenya walikuwa na matumaini kwamba Mkuu wa Nchi angetimiza ahadi yake lakini familia zimeendelea kuwapoteza wapendwa wao kwa mtindo sawia.

Malalamiko haya yaliibuliwa na mashirika ya haki za binadamu na wabunge mbalimbali wanaotaka uchunguzi wa haraka na wa uwazi kuhusu kesi hizi, uwajibikaji kwa waliohusika, na hatua madhubuti za kuzuia matukio zaidi.

Rais William Ruto alivunja SSU mwaka jana, kikosi cha polisi kilichoaminiwa kutekeleza mauaji ya kiholela na utekaji nyara kwa watu mwaka jana.

Alitaja uamuzi huo kuwa ni hatua nzuri ya kushughulikia masuala ya muda mrefu ya ukatili wa polisi na ukiukaji wa haki za binadamu na kuzuia ukatili zaidi.

Aidha, kutoweka kwa hivi majuzi kwa watu katika sehemu mbali mbali nchini kumezua wasiwasi huku familia na wabunge wakiomba kuingilia kati kwa serikali.

Ripoti kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu, akiwemo Afisa wa masuala ya dharura wa shirika la Haki Africa, Bw Mathias Shipeta, zinaonyesha matukio ya kusikitisha.

Kulingana na mwanaharakati huyo wa haki za binadamu, ndani ya muda wa wiki moja, visa vinne vya kutoweka kwa watu kwa njia ya kutatanisha  vilirekodiwa katika eneo la pwani pekee.

“Rais alibainisha kuwa utekaji nyara kwa nguvu utakomeshwa, nini kinaendelea? Tunaiomba serikali iingilie kati na kutafuta njia. Kati ya kesi nne ambazo tumepokea, moja ilikuwa ya Lamu na tatu katika Kaunti ya Mombasa,” alisema Bw Shipeta.

Uchunguzi wa Taifa Leo umefichua hali hii si eneo la Pwani pekee bali visa kama hivi vimeshuhudiwa katika maeneo mengine ya nchi ukiwemo mji mkuu wa Nairobi.

Wabunge katika eneo lililoathirika wameingilia kati wakimtaka mkuu wa nchi kutimiza ahadi yake.

Akiwa Bungeni wiki hii, Mbunge wa Garissa Meja Dekow Barrow aliibua wasiwasi kufuatia ongezeko la visa vya utekaji nyara katika eneo bunge lake.

Mbunge Dekow alibainisha bungeni kuwa familia za watu hawa waliopoteza jamaa zao zinakabiliwa na sintofahamu kuhusu waliko wapendwa wao.

Mbunge Maalum wa Garissa Bi Umulkheir Harun wakati wa mahojiano katika televisheni alisema, “Kufikia mwezi huu, vijana wanne wametekwa nyara kutoka kaunti yangu. Tumeomba majibu kutoka kwa wakuu wa usalama lakini ilibidi tuweke shinikizo zaidi na watatu waliachiliwa. Utawala huu mahususi ulifanya kampeni ya kuwalinda vijana lakini hatuoni hilo,” alisema Mbunge Harun.

Jijini Nairobi, takribani watu watano wameripotiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha katika muda wa wiki moja iliyopita. Kisa cha hivi punde zaidi ni cha Osman Khalif, rafiki wa karibu wa Gavana Johnson Sakaja ambaye alitoweka wiki jana Ijumaa.

Watu watano wenye silaha wanaripotiwa kutumia gari na kumteka nyara Khalif ndani ya Kituo cha kibiashara cha Sarit katika kitongoji cha Westlands siku ya Ijumaa mwendo wa saa kumi na moja jioni.

Wabunge hao wanataka kukomeshwa kwa visa hivi vya utekaji nyara,  kulingana na wao magari yasiyo na nambari ya usajili hutumiwa na watekaji nyara wanaoshukiwa kuwa maafisa wa polisi.

Kutoweka na kujitokeza tena ghafla kwa baadhi yao kumewafanya Wakenya kushangaa huku wengi wakikataa kuzungumzia masaibu yao ya kutekwa nyara.

 

  • Tags

You can share this post!

Nilimpa demu jirani lifti akiwa mlevi, sasa amenigandia...

Jinsi mhasibu wa benki alichoma Sh1 milioni katika uraibu...

T L