• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Jinsi mhasibu wa benki alichoma Sh1 milioni katika uraibu wa kamari na kubakia na majuto

Jinsi mhasibu wa benki alichoma Sh1 milioni katika uraibu wa kamari na kubakia na majuto

NA FRIDAH OKACHI

MHASIBU Mbugua Karanja alitumia zaidi ya Sh1 milioni za benki kwenye mchezo wa kamari. Uraibu huo ni baada ya mwajiri wake kumpa muda wa kupunguza unywaji wa pombe.

Bw Karanja, 33, alianza mchezo wa kamari  baada ya mwajiri wake kumpa muda wa mapumziko ili apate nafasi ya kurekebisha tabia kutokana na unywaji pombe kupita kiasi. Unywaji huo akianza akiwa na umri wa miaka 14 hadi alipoajiriwa.

“Nilimaliza nikiwa mdogo, niliendelea na hali hiyo hadi chuo kikuu. Baadaye nilipata kazi katika benki moja kama mhasibu. Uhuru wa kutumia pesa zangu ninavyotaka ulinifanye nizame zaidi katika uraibu wa pombe na ikabidi mwajiri anipe muda niweze kutatua tatizo langu,” alianza kusimulia.

Katika kipindi cha miezi hiyo mitatu, aliwacha unywaji wa pombe na kuanza kucheza kamari hadi akawa mraibu.

Akizungumza na Taifa Leo Digitali, alisema alianza kama shabiki wa kucheza bila kufahamu atakuwa mraibu na baadaye akose kazi.

“Nilianza kama shabiki, nikicheza, nawekea Man U, Arsenal, Chelsea…Kichwa. Lakini kuendelea nikawa mraibu sasa. Wakati huo nilipoteza Sh 1.2 milioni kando na hiyo nikapoteza kazi,” alisema Mbugua.

“Nilikuwa nachukua 50, 100 nacheza nazo kubeti…  Kwa kipindi cha miaka miwili nilikuwa nimetumia Sh1 milioni na zaidi, unajua ukiwa pale ndani nilikuwa nachanganya meneja wangu, nikiwa ninatoa huku na kupeleka pale haikuwa rahisi kujulikana,” aliendelea.

“Benki hiyo ilinishtaki, nilikaa mle ndani nikisubiri famiia yangu kuuza shamba kulipa pesa hizo. Kulikuwepo na maelewano familia yangu kulipa pesa hizo ili niwe huru,” alisema Bw Karanja.

Wakati huo akiwa kwenye rumade, familia yake iliuza shamba na kurudishe kiwango alichotumia.

Bw Karanja ambaye sasa amebadilika na kuwa mshauri nasaha, alisema mchezo wa kamari sio tatizo la kifedha. Shida ikiwa ni fikira na hisia ambazo wengi hujaribu kuponya. Hamu ikiwa ni kutatua matatizo yanawaandama.

“Kuna siku nilipata Sh224,000 kupitia mchezo huo. Lakini sikuwacha niliendelea nikijua nitapata Sh1 milioni au zaidi kutatua shida zangu. Hali haikua sawa hadi nilipofika kiwango cha kuwa maskini zaidi,” alisema Bw Karanja.

Mchezo huo ulizidi na kushindwa kujikimu kifedha na kuingilia kuuza vitu vyake kama vile viatu, nguo zake hadi kuuza duka lake ya kinyozi.

Hali hiyo ilimsababishia kupoteza mke na mtoto kutokana na tatizo hilo.

“Mke aliniacha, aliona siwezi mhudumia matumizi ya nyumbani. Kazi iliisha na kufikia sasa sijawahi pata fursa ya kurudiana na familia yangu,” alisema Bw Karanja.

  • Tags

You can share this post!

Ahadi ya Ruto kukomesha utekaji nyara yageuka hewa kesi...

Makaburi mapya yafichuka Shakahola na kurudisha darubini...

T L