• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Abuni apu ya ‘Mkulima Young’ inayosaidia wakulima kuuza bidhaa zao

Abuni apu ya ‘Mkulima Young’ inayosaidia wakulima kuuza bidhaa zao

NA PETER CHANGTOEK

MARA nyingi, wakulima wamekuwa wakiyazalisha mazao ya shambani lakini hawapati soko la kuuzia.

Ni kwa muktadha huo, ambapo mkulima mmoja, ambaye pia ni msomi, aliwaza na kuwazua kuhusu jinsi ambavyo angewasaidia wakulima kupata soko.

Dkt Joseph Macharia akaamua kubuni apu ambayo huwasaidia wakulima kuuza mazao hayo. Apu hiyo inajulikana kama Mkulima Young.

Wakulima hutangaza bidhaa zao bila malipo kwa apu hiyo, kwa kupakia picha za mazao na wateja wanaopendezwa na bidhaa zenyewe, huwasiliana na muuzaji na kuzinunua.

Dkt Macharia, ambaye pia ni mkulima, alisomea Shahada ya Kilimo katika Chuo Kikuu cha Egerton, kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), kwa Shahada ya Uzamili, na hatimaye kusomea Shahada ya Uzamifu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Queensland, Australia.

Alijiwa na wazo la kubuni apu hiyo miaka sita iliyopita, na akaibuni miaka miwili baada ya kujiwa na wazo lenyewe.

“Kwanza, niliamua kuunda jukwaa hilo kwa sababu ya historia yangu ya kilimo na kusomea kilimo, na niliona ni muhimu kusaidia jamii. Pili, nilitumia yale niliyokuwa nimesomea kutengeneza jukwaa ambalo wakulima watalitumia kusuluhisha tatizo la kupata soko na kupata habari kuhusu bidhaa za kilimo, na kuwatia shime vijana kujihusisha na kilimo,” aeleza.

Anasema kuwa, wale wanaotaka kuuza bidhaa zao, hupakia picha na maelezo ya mazao au bidhaa wanazoziuza kwa Mkulima Young.

Wanaonuia kulitumia jukwaa hilo, wanafaa kujisajili au kupakua apu hiyo kutoka kwa Google Play Store, ili wapate uwezo wa kutangaza bidhaa zao.

“Apu hiyo hupatikana kwa Google Play Store. Hata hivyo, huwasihi watumiaji kujisajili kwa tovuti,” asema Dkt Macharia, ambaye mara nyingi hukaa Australia.

Dkt Joseph Macharia akiwa na ng’ombe wake, Australia. PICHA | HISANI

Anafichua kwamba, takriban watu 45,000 wamejisajili kuitumia apu hiyo, na takriban watu 1,000 huingia kwa tovuti hiyo kila siku.

Ili kuhakikisha kuwa data za watumiaji zinahifadhiwa vyema, bila kuibwa na kutumiwa vibaya, wao huzingatia sheria za Kenya za kulinda data (KDPA).

“Huku imani ikiwa muhimu katika jukwaa lolote la mitandaoni, tumeweka maelekezo kuhusu jinsi ya kulitumia. Zaidi ya hayo, tuna sheria na masharti,” adokeza.

Anasema kuwa, watumiaji wanafaa kuwa na simu za kisasa. Hata hivyo, ameshuhudia wale wasiokuwa na aina hizo za simu, wakitangaziwa bidhaa kwa niaba yao, na wale walio na simu hizo.

Anaongeza kuwa, watu wengi walianza kulitumia jukwaa la Mkulima Young, wakati janga la Covid-19 lilipoingia nchini.

Kwa mujibu wa Dkt Macharia ni kuwa, madhumuni yake makuu alipokuwa akibuni apu hiyo yalikuwa ni kuhakikisha kuwa wakulima wanapata suluhisho ya tatizo la kupata soko.

Anasisitiza kuwa, Mkulima Young “ilibuniwa na mkulima kwa ajili ya wakulima”, na ana nia ya kupanua matumizi yake nje ya ukanda wa Afrika Mashariki.

  • Tags

You can share this post!

Vishale: Maafande wa Nakuru Mashariki ndio mabingwa wa taji...

CHAKULA CHA UBONGO: Njia za kujituliza unapotengwa na watu...

T L