• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
AFC yakabiliwa na changamoto kufadhili kilimo

AFC yakabiliwa na changamoto kufadhili kilimo

Na RICHARD MUNGUTI

 SHIRIKA la Kufadhili Kilimo Nchini (AFC) linakabiiliwa na changamoto za kutoa mikopo kwa wakulima kununua pembejeo za kilimo.

Ukosefu wa pesa za kutosha kufadhili kilimo utavuruga mpango wa serikali wa kuzalisha chakula cha kutosha.

Asasi hii ya serikali hupokea maombi ya mikopo ya kima cha Sh15 bilioni kwa mwaka lakini imekuwa ikitoa mikopo ya Sh4 bilioni na kupelekea idadi kubwa ya wakulima kukosa pesa za kununua mbolea na bidhaa nyinginezo.

“Idadi kubwa ya maombi ya mikopo imepita kiwango cha pesa kilichoko katika AFC. Hata hivyo, mipango inafanywa kuona jinsi washirika wetu watasaidia kuwafadhili wakulima,” alisema Bw George Kubai, Mkurugenzi AFC, wakati wa mahojiano huku akikiri uhaba wa pesa unaathiri uzalishaji kilimo.

Bw Kubai alisema wakulima hawajalipa mikopo ya Sh1.2 bilioni.

Aliwataka wanaodaiwa walipe mikopo hiyo ili wakulima wengine wafaidi.

“AFC hutoa mikopo kwa kiwango cha riba ya asilimi mia 10 ambacho ni cha chini mno kikilinganishwa na mashirika mengine ya kifedha yanayotoza riba ya juu,”alieleza Bw Kubai kwa njia ya simu.

Wakulima wengi katika eneo la North Rift wameiomba serikali ifadhili AFC kuwezesha watu wengi kufaidika na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Baadhi ya wakulima wamesema kwamba hawajapata mikopo licha ya kulipa mikopo ya awali.

“Licha ya kwamba AFC inakabiliwa na changamoto za fedha, inatakiwa kutoa mikopo kwa wakulima kutokana na pesa zilizolipwa,”alisema Amos Chirchir, ambaye ni mkulima kutoka Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.

Zaidi ya wakulima 200 wa mazao ya nafaka katika eneo hilo linalozalisha chakula kwa wingi waliomba mikopo kabla ya msimu wa kupanda kuanza.

“Itabidi wakulima wengi wapunguze ekari walizotenga kupanda kwa kukosa fedha za kutosha kununua mbolea na mbegu.

“Upunguzaji huu utakinzana na mwongozo wa serikali wa kuhakikisha kuzalisha chakula cha kutosha kukimu mahitaji ya Wakenya,” alisema mkurugenzi wa ADC Bw Kipkorir Menjo.

Bw Menjo alilalama sekta hii ya uuzaji mbegu na mbolea imeingiliwa na mabroka wanaouza bidhaa za kilimo kwa bei ya chini.

Viongozi na wakulima wameomba serikali ipunguze bei ya mbolea kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao.

Wakulima na viongozi wamesisitiza bei ya mbolea ya Calciums Ammonium Nitrate (CAN) ipunguzwe kutoka Sh3, 500 hadi Sh2, 500.

Wakiongozwa na Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago, viongozi hao wamemsihi Rais William Ruto kupunguza bei ya CAN kutoka Sh3, 500 hadi Sh2, 500 ndiposa wakulima waweze kuinunua.

“Hakuna namna wakulima watanunua mbolea ya kupanda na ile ya CAN kwa bei moja kwa bei ya Sh3, 500. CAN ipunguzwe hadi Sh2, 500,” alisema Bw Mandago.

Bodi ya nafaka NCPB ilikuwa inauza mbolea ya CAN kwa bei ya Sh1, 950 lakini ikaongezwa hadi Sh3, 500.

Kutokana na uhaba wa mbolea, uzalishaji wa mahindi katika eneo la Rift valley umepungua kutoka magunia 27 milioni hadi 21 milioni msimu uliopita.

Viongozi hao walitoa wito huo Rais Ruto alipozuru Uasin Gishu.

Nchi hii inahitaji tani 650, 000 za mbolea kila mwaka.

 

  • Tags

You can share this post!

Marais waalikwa wafuatilia hafla kwenye runinga

Wafugaji washtakiwa kwa wizi wa mifugo Nairobi

T L