• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Daktari aonya wanaume wa kuendea madoli

Daktari aonya wanaume wa kuendea madoli

NA MWANGI MUIRURI

MSIMAMIZI mkuu wa hospitali ya Murang’a Dkt Leonald Gikera amewaonya wanaume wanaoendea madoli ya ngono akisema wanapofanya hivyo kwa awamu, wanajiweka kwa hatari kubwa.

Dkt Gikera amesema endapo wanaonufaika na huduma hizo hawatumii mipira ya kujikinga dhidi ya magonjwa, basi wanaweza kuambukizana maradhi ya zinaa.

Amesema hayo wakati mdokezi ameambia Taifa Leo kwamba kilabu kimoja mjini Murang’a kimetoa bonasi kwa baadhi ya wateja wake wa kiume kwa kuwaletea madoli ya ngono.

Kilabu hicho kinasifika kwa kuandaa densi za watu kujiachia wakiwa uchi wa mnyama.

Mdokezi mmoja amesema kilianza kutoa huduma hizo bila malipo mnamo Desemba 20, 2023, hali ambayo itaendelea hadi Januari 2, 2024.

“Kuna madoli matano ambayo yamewekwa kwa chumba kimoja katika baa hiyo kwa lengo la kuwapa wanaume burudani,” akasema mdokezi mmoja ambaye ameshabikia hali hiyo bila kujali hatari iliyoko.

Lakini Dkt Gikera amesema uchafu unaoweza kuwa katika mazingara hayo ya mahaba ni mwingi sana na “kamwe ni hali isiyokubalika katika viwango vya afya ya umma”.

“Hiyo ni hatari kubwa sana kwa kuwa walevi wakiingia kwa mahaba ya aina hiyo bila kinga, huenda waambukizane maradhi ya zinaa,” akasema Dkt Gikera.

Ingawa hivyo, amesema ni biashara ya wenyewe ambayo imepewa leseni na mamlaka mbalimbali chini ya vigezo vya burudani na itabidi atokee mlalamishi ndipo uchunguzi ufanywe kuhusu hilo.

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu alisema kwamba “mambo kama hayo yanaweza tu yakaendelezwa chini ya utepetevu wa Idara ya Afya ya Umma iliyo chini ya serikali ya Kaunti pamoja na Idara ya Usalama”.

“Huo ni uchafu na hali ya kusababisha mlipuko wa maradhi kando na kuwa taka kwa kuzingatia mila za wenyeji,” akasema seneta Nyutu.

Bw Nyutu alisema mwenye kuleta vinyago hivyo amedhihirisha kwamba anawadharau na kuwadunisha huku fikira zake zikiwa ni za pesa tu.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kwamba bei zote za pombe katika baa hiyo zimeongezwa kwa kati ya Sh50 na Sh70 kwa zile za chupa huku zile za makali zikipigwa nyongeza ya kati ya Sh150 na Sh250.

Hatua hiyo ya kuingiza madoli imetafsiriwa kuwa kivutio kwa wateja ambao wakilia kuhusu bei za juu, basi wanajituliza kwa madoli ya mahaba.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wakenya wapimiwa umeme kama dawa

Chapati Festival: Krismasi ya mapema Riruta

T L