• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:42 PM
Mwanamume aliyepooza kwa sababu ya Polio asimulia jinsi alivyoacha shule kwa kuchekwa na wenzake

Mwanamume aliyepooza kwa sababu ya Polio asimulia jinsi alivyoacha shule kwa kuchekwa na wenzake

NA KALUME KAZUNGU

KILA anaposimama kuzungumza, iwe ni kwenye makongamano, mikutano au hata  kampeni zinazofungamana na afya, hasa suala la chanjo na ugonjwa wa polio kwa ujumla, Bw Abdulbar Ali Kassim huishia kububujikwa na machozi na mara nyingine hata kukatiza hotuba zake.

Hili linatokana na kumbukumbu ya masaibu aliyopitia zaidi ya miongo minne iliyopita baada ya ugonjwa wa polio kumvamia na kumtafuna bila huruma.

Bw Abdulbar, mkazi wa kisiwa cha Lamu, kwa sasa ana miaka 51.

Alizaliwa akiwa buheri wa afya, ambapo viungo vyake vyote vya mwili havikuwa na kasoro yoyote.

Alipotinga umri wa miaka mitatu, Bw Abdulbar aliambukizwa polio, hali iliyomwacha na ulemavu kwenye mguu wake wa kulia.

Kwa sasa yeye ni kiguru.

Ikumbukwe kuwa polio ni ugonjwa wa kuambukiza wa mishipa katika uti wa mgongo unaosababisha kupooza kwa viungo vya mwili na mfumo mzima wa neva kwa ujumla.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Abdulbar aliutaja ugonjwa wa polio kuwa doa jeusi lililogubika maisha yake na kuyafanya kukosa maana kabisa.

Anasema baada ya kupona, wazazi wake walimpeleka shuleni kuanza safari yake ya elimu, wakitarajia kwamba angehitimu masomo yake ya msingi na kujiunga na sekondari, chuo kikuu na kisha kupata kazi nzuri ya kujikimu maishani na pia kusaidia wazazi.

Alijiunga na shule ya msingi ya wavulana ya Lamu mnamo mwaka 1987.

Ni wakati huo ambapo Bw Abdulbar alianza kukerwa na kejeli za kila siku kutoka kwa wanafunzi wenzake kuhusiana na ulemavu wake uliotokana na athari za polio.

Anasema kila alipotembea kwa kuchechemea, wanafunzi walikuwa wakimchekelea kwa masihara.

Kuna walionong’onezana chini kwa chini kila alipopita mahali ilhali kuna wale waliokuwa wakimtupia cheche za dhihaka paruwanja kuhusu hali yake.

“Karibu kila mwanafunzi alikuwa amenibandika jina la kiguru. Kuna ambao hawakutaka hata kuandamana au kutembea nami kwa sababu ya ulemavu uliosababishwa na polio. Wanafunzi shuleni walikuwa wamenigeuza kuwa chemichemi ya kicheko. Ni jambo lililoniudhi na kunitatiza akili sana. Nikawakasirikia wananfunzi na shule nzima kwa ujumla,” akasema Bw Abdulbar.

Mnamo mwaka 1992, akiwa darasa la sita, Bw Abdulbar alichoshwa na dhihaka za wanafunzi shuleni.

Akaamua potelea mbali. Elimu wacha ikae.

Alikatikza masomo yake akijua fika kuwa angalau atapata faraja nafsini mwake akiwa amejifungia nyumbani ambako hakuna wa kumcheka au kumsuta kama alivyokuwa akishuhudia shuleni.

Juhudi za wazazi wake kujaribu kumrai kurudi shule kuendeleza masomo yake ziligonga mwamba.

“Hivyo ndivyo masomo yangu niliyakatiza. Nilikaa nyumbani, ambapo muda mwingi niliupitisha nikiwa nimejifungia chumbani mwangu ilmradi nisionekane na waja na kuchekelewa,” akasema Bw Abdulbar.

Bw Abdulbar aidha anajutia maamuzi yake kwani yamemfanya kuishi katika hali ya uchochole.

Yeye ni baba wa watoto tisa.

Ana mabibi wawili na amekuwa akiikimu familia yake kwa kutegemea kazi za kijungujiko, ikiwemo unahodha wa boti na mashua za kubeba abiria kisiwani Lamu.

“Hadi leo najutia maamuzi yangu ya kuacha shule kwa sababu ya unyanyapaa niliopata kutokana na ulemavu unaotokana na polio. Ninaendesha maisha magumu. Ninaamini ningepuuzilia mbali kejeli za wenzangu shuleni na kuendeleza elimu yangu hadi chuo kikuu kwa sasa ningekuwa afisa wa ngazi za juu katika bodi ya walemavu nchini. Nachukia polio na unyanyapaa hadi leo,” akasema Bw Abdulbar.

Kwa sasa yeye ndiye balozi wa masuala yanayofungamana na maradhi ya polio na chanjo katika idara ya afya ya umma kaunti ya Lamu.

Bw Abdulbar Ali Kassim, mkazi wa kisiwa cha Lamu mwenye umri wa miaka 51 ambaye alitoroka shule akiwa katika Darasa la Sita baada ya kushindwa kuvumilia kejeli kutoka kwa wanafunzi wenzake kutokana na athari za polio. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anasema kutokana na masaibu yake, kamwe hawezi kuiacha jamii kuendelea kupuuzilia mbali suala la chanjo ya polio, akiapa kuendeleza kampeni ya nyumba hadi nyumba kuelimisha waja kuhusiana na umuhimu wa chanjo ya polio.

“Kuna watu wamekuwa wakiingiza dhana zisizo na msingi kuhusiana na chanjo ya polio. Mimi siwezi kuruhusu jamii yangu kupotoshwa na kupuuza hili suala la chanjo ya polio kwa watoto wa chini ya miaka mitano hasa kutokana nay ale niliyapata udogoni mwangu. Lazima wazazi wawe mstari wa mbele kuwaruhusu watoto wao kuchanjwa polio ili kupunguza idadi ya walemavu Lamu na nchini kwa ujumla,” akasema Bw Abdulbar.

Kwa upande wake, Afisa wa Mawasiliano na Matangazo katika Idara ya Afya ya Umma, Kaunti ya Lamu, Ahmed Muhsin alimtaja Bw Abdulbar kuwa kiungo muhimu cha jamii na idara ya afya ya umma eneo hilo kwa ujumla katika kukabiliana na maradhi ya polio.

Bw Muhsin anasema ni kupitia kwa juhudi za Idara ya Afya ya Umma kwa ushirikiano na Bw Abdulbar, ambapo idadi kubwa ya watoto wamekuwa wakipokezwea chanjo ya polio mara kwa maera kote Lamu.

“Twamshukuru Bw Abdulbar kwa kujitolea kwake kuwa balozi wa chanjo ya polio Lamu. Idara yetu imekuwa ikimtumia sana Bw Abdulbar kuelezera jamii kuhusu athari za polio, ambapo yeye mwenyewe ni mwaathiriwa wa ugonjjwa huo. Ametusaidia pakubwa kuirai jamii kukubali mpango wa chanjo na kuondoa dhana potovu miongoni mwa jamii ya Lamu kuihusu hii chanjo ya polio,” akasema Bw Muhsin.

Naye Afisa Mkuu wa Masuala ya Utafiti wa Maradhi Kaunti ya Lamu, James Mbugua alisema ipo haja ya jamii ya Lamu kukumbatia chanjo ya polio kila mara inapotolewa, ikizingatiwa kuwa eneo hilo limezingirwa na kaunti ya Garissa nan chi ya Somalia ambapo visa vya maradhi ya polio vimekuwa vikigunduliwa.

“Lamu iko mpakani mwa kaunti ya Garissa na pia nchi jirani ya Somalia. Kule Garissa tayari kuna visa vinane vinavyoshukiwa kuwa vya polio. Uchunguzi wa kina kuvihusu visa hivyo unaendelea. Ni matumaini yangu kwamba wakazi wa Lamu watakumbatia chanjo inayotolewa kila mara ya polio kwa kuhakikisha watoto wao wa chini ya umri wa miaka mitano wanachanjwa ili kuzuia maambukizi ya maradhi hayo hatari,,” akasema Bw Mbugua.

Katika awamu ya kwanza iliyozinduliwa Jumamosi, Lamu inalenga jumla ya watoto 26,400 kuchanjwa dhidi ya polio.

Shughuli hiyo itatekelezwa kwa siku tano mfululizo.

Awamu ya pili ya zoezi hilo inatarajiwa kung’oa nanga mapema Novemba 2023.

  • Tags

You can share this post!

Babu Owino asuta Ruto kwa maamuzi kupeleka polisi wa Kenya...

Kalonzo awatetea Mutua na Malonza kwa kushushwa vyeo

T L