• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Wagonjwa wa kansa taabani mashini za KNH zikipata hitilafu

Wagonjwa wa kansa taabani mashini za KNH zikipata hitilafu

Na ANGELA OKETCH

MAELFU ya wagonjwa ambao walikuwa wakitibiwa kansa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), watalazimika kusubiri kwa muda mrefu, kufuatia mzozo kati ya hospitali hiyo na kampuni iliyotarajiwa kukarabati mitambo inayotumika kutibu ugonjwa huo.

Mitambo miwili ya radiotherapy, ambayo imekuwa ikitegemewa kuwatibu wagonjwa wa kansa katika hospitali hiyo, haijafanya kazi kwa muda wa wiki sita zilizopita.

Kulingana na afisa mmoja katika KNH aliyezungumza na Taifa Leo, usimamizi umeagiza vipuri vya mashine hizo.

“Tunasubiri vipuri hivyo viwasilishwe ili iweze kukarabatiwa. Mambo yatakuwa shwari ndani ya wiki chache zijazo,” akasema.

Awali, usimamizi wa hospitali hiyo ya rufaa ilisema kuwa walikuwa wakisubiri kampuni iliyotengeneza mashine hizo kutuma mafundi wa kuikarabati mashine hiyo, lakini haikutimiza ahadi hiyo.

Imeibuka kuwa hospitali ya KNH na kampuni hiyo ya kutoka India, haikukubaliana kuhusu upande ambao utagharamia usafiri wa wahandisi hao.

Haikujulikana kama kulikuwa na mkataba kati ya hospitali hiyo na kampuni hiyo kuhusu suala zima la ukarabati wa mashine hizo.

Wagonjwa wengi wa kansa hupenda kusaka huduma za matibabu katika KNH kwa sababu ada zake sio ghali ikilinganishwa na hospitali zingine nchini.

Wale ambao walisafiri kutoka maeneo ya mbali, huketi kila siku katika hospitali hiyo wakisubiri mitambo hiyo ikarabatiwe. Wamesalia pweke na wasiwasi mkuu wasijue la kufanya.

Wakati huu, ikiwa mgonjwa atapimwa katika KNH na kupatikana na kansa, atalazimika kusubiri kwa muda wa miezi sita kabla ya kuwekwa katika orodha ya wagonjwa wa kutibiwa.

Kutokana na tatizo hilo, hospitali hiyo sasa haiwakubali wagonjwa wapya, kutokana na hitilafu za mitambo ya tiba.

Data katika KNH zinaonyesha kuwa wagonjwa wamesajiliwa kwa matibabu hadi Aprili mwaka ujao.

Lakini sasa hospitali hiyo inajaribu kuwaorodhesha kwa matibabu kwa kutumia mashine moja iliyosalia.

“Nilianza matibabu yangu mwaka 2021 na nilipofika KNH kwa awamu ya matibabu mnamo Desemba 27, 2021, niliambiwa mashine zina hitilafu. Niliagizwa kurejea Januari 3, 2022. Niliporejea, nilishauriwa nirejee nyumbani nisubiri simu kutoka kwa usimamizi wa hospitali,” akasema Bi Millicent Awino ambaye anaugua saratani ya matiti.

Rafiki yake alimpa hifadhi, Nairobi, lakini baada ya siku tatu, hakuwa amepata simu kutoka KNH.

Hatimaye aliamua kurejea nyumbani Webuye.

Bi Awino anaugua kansa ya matiti. Ana wasiwasi kwamba seli za kansa hiyo huenda zikaenea katika sehemu zingine za mwili.

“Kwa sababu sasa sipati matibabu, ninahisi uchungu kwa sababu hakuna wa kushughulikia vidonda vyangu na hali hii inaathiri afya yangu,” akasema.

Kuna wagonjwa wengi wa kansa ambao wanapitia masaibu sawa nay ale yanayomzonga Bi Awino, kutokana na kuharibika kwa mishine za kutibu ugonjwa huo katika KNH.

  • Tags

You can share this post!

Raila awahimiza Wakenya washirikiane bila kujali kabila,...

Haaland aongoza Dortmund kuponda Freiburg katika gozi la...

T L