• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Raila awahimiza Wakenya washirikiane bila kujali kabila, rangi

Raila awahimiza Wakenya washirikiane bila kujali kabila, rangi

Na WANGU KANURI

KIONGOZI wa Azimio la Umoja, Raila Odinga amewaahidi wafuasi wake waliokongamana katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya, Thika, leo Jumamosi kuwa yeye na Rais Uhuru Kenyatta, hawataruhusu matendo au maneno yatakayovuruga amani nchini Kenya.

Akirejelea matamshi ya Seneta Mithika Linturi ya ‘madoadoa’, Bw Odinga alisema kuwa kila Mkenya ana uhuru wa kuishi pahali popote nchini bila kuhangaishwa na yeyote.

“Tuko hapa sio kwa ajili ya mwaliko kutoka mtu yeyote. Tuko hapa kwa sababu sisi sote ni Wakenya,” akasema.

Bw Odinga pia alimsifia Rais Kenyatta kwa utendakazi wake huku akieleza kuwa kazi alizofanya bado zitaendelea hata akiondoka mamlakani.

Hata hivyo, kinara huyo wa ODM alihakikisha kuwa Mpango wa Maridhiano (BBI), haujafa na utaendelea kwani unanuia kuyainua maisha ya Wakenya.

Akishukuru viongozi wa Kiambu kwa kumkaribisha, Bw Odinga alieleza kuwa iwapo BBI ingefanikiwa, kaunti hiyo ingepata bilioni 9.

“Nimesikia vijana wanasaka nafasi za ajira, mama mboga waweze kujiendeleza kibiashara, wakulima wawezeshwe kukuza vyakula vyao na walemavu wasisahauliwe,” akasema.

Huku msafara wa Azimio ukiwa mjini Thika, Naibu Rais William Ruto kesho Jumapili atakuwa katika uwanja wa Jacaranda, Embakasi Mashariki.

You can share this post!

KPA yashindwa kusimamisha kesi dhidi ya mkurugenzi mkuu

Wagonjwa wa kansa taabani mashini za KNH zikipata hitilafu

T L