• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Aina mpya ya nyasi za mifugo yenye ubora wa hali ya juu

Aina mpya ya nyasi za mifugo yenye ubora wa hali ya juu

NA SAMMY WAWERU

CHINI ya kipindi cha muda wa miaka mitatu mfululizo, wafugaji nchini wamekuwa wakipitia hali ngumu kutokana na gharama ya juu ya malisho.

Ni hali ambayo imechochea biashara ya ufugaji kuwa ngumu, baadhi wakilazimika kupunguza kiwango cha mifugo na wengine kusitisha biashara.

Chakula cha mifugo kinazidi kuwa ghali, licha ya serikali kuahidi kuangazia mfumko wa bei.

Kulingana na Muungano wa Viwanda vya Kutengeneza Malisho ya Mifugo Nchini (Akefema), kuendelea kukosekana kwa malighafi ndio chanzo cha gharama kuwa ghali.

Kenya huagiza kutoka nje zaidi ya asilimia 80 ya malighafi ya chakula cha mifugo.

Mary Njeri ambaye ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa, hata hivyo amevumbua aina ya nyasi mpya inayomuondolewa kero ya bei.

Akiwa mfugaji eneo la Tetu, Kaunti ya Nyeri, Njeri anasema tangu aanze kukuza Pakchong 1 Super Napier amekwepa changamoto zinazozingira wakulima wenza.  

Mary Njeri, akielezea kuhusu aina mpya ya nyasi –  Pakchong 1 Super Napier. PICHA | SAMMY WAWERU

Ikiwa na asili ya Thailand, nyasi hiyo imetokana na kujamiishwa kwa mabingobingo ya kawaida (napier) na mtama wa lulu (pearl millet).

“Ina asilimia 18 ya madini ya Protini, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kikilinganishwa na vyakula vingine vya mifugo,” Njeri adokeza.

Awali, mama huyu alikuwa na jumla ya ng’ombe wanne ila alilazimika kuwapunguza 2020 hadi wawili kwa kile anataja kama “kulemewa na gharama ya malisho”.

Aligundua kuhusu Pakchong 1 Super Napier mwaka uliopita, kupitia maonyesho ya kilimo Eldoret, ASK.

“Nilikuwa nikitumia wastani wa Sh880 kila siku kugharamia chakula, bei ambayo imepungua hadi Sh150 kwa ajili ya nyasi hii mpya,” aelezea.

Aidha, anaikuza kwenye ekari moja.

“Huvuna baada ya miezi miwili na nusu ya upanzi, kisha ninaipa ng’ombe.”

Kando na kuwapa nyasi mbichi zilizokatwakatwa vipande, pia huunda hay na silage.

Mfugaji Mary Njeri akionyesha Pakchong 1 Super Napier wakati wa Maonyesho ya Kimataifa ya Kibiashara na Kilimo Nairobi (ASK), mwaka huu 2022. PICHA | SAMMY WAWERU

Hupiga jeki malisho kwa virutubisho faafu, Njeri akisema kiwango cha uzalishaji maziwa kimeongezeka kutoka lita 8 hadi 20 kwa siku.

Hali kadhalika, mfugaji huyu huuzia wakulima wenzake kwa minajili ya kuzalisha.

Kabla kupandwa, mbegu zake (matawi) zinapaswa kutibiwa na HB-101 Plant Vitalizer. 

Njeri aidha alikuwa miongoni mwa wawekezaji katika sekta ya kilimo na ufugaji waliohudhuria Maonyesho ya Kimataifa ya Kibiashara na Kilimo Nairobi (ASK), mwaka huu 2022.

  • Tags

You can share this post!

Rais atoa ahadi zaidi kwa mahasla

Raila na Ruto kukutana leo Jumanne katika kongamano la...

T L