• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Haya machenza ya kwake yanasubiri kuchumwa tu!

Haya machenza ya kwake yanasubiri kuchumwa tu!

Na PETER CHANGTOEK

KAUNTI ya Makueni inatambulika mno nchini kwa ukuzaji wa mimea ya matunda, kama vile michenza, miembe na michungwa. Matunda hayo yamekuwa kitegauchumi kwa wakulima wengi katika kaunti hiyo.

Benson Mbithe ni mmojawapo wa wakulima wanaochuma hela kutokana na kilimo cha machungwa na machenza.

Unapoingia katika shamba lao lililoko katika eneo la Katulyani, eneobunge la Kibwezi Magharibi, utadondokwa na mate kwa kutamani kuyala matunda mabivu, yanayoning’inia kwa miti.

Benson Mbithe akiwa katika shamba lao la michungwa na michenza, katika kitongoji cha Katulyani, Kibwezi West, Kaunti ya Makueni. Picha | Peter Changtoek

Katika shamba lao la ekari mbili, Mbithe na wazazi wake huikuza mimea zaidi ya 400, shughuli waliyoanza miaka kadhaa iliyopita.
“Tulianza kuikuza mimea miaka saba iliyopita; inachukua muda kukua. Tunapanda ‘pixie’, michungwa, midimu, na miembe, pia kuna mipapai,” asema.

“Tulinunua miche kutoka mahali panapoitwa Kalamba, Matiliku. Mmoja huuzwa Sh30,” aongeza mkulima huyo.

Kabla hawajapanda miche, wao hulitayarisha shamba vyema kwa kufyeka na kulima. “Unahakikisha kwamba shamba limefyekwa.

Tunatumia mbolea za kawaida za ng’ombe tu. Tunachukua hapa tu, huwa hatununui,” aongeza.

Anadokeza kuwa, baada ya kulitayarisha shamba, wao huyachimba mashimo ya kuipandia miche. Mashimo hayo, asema, huwa ni futi tatu kwa upana na futi nne kwa kina.

Mbithe anasema, baada ya kuchimba mashimo hayo, huchanganya mbolea na udongo uliochimbuliwa kutoka kwa mashimo na kumwagia maji, kabla hawajaipanda miche ya michungwa na michenza.

Anafichua kuwa, baada ya kuipanda miche, huchukua muda wa miaka mitatu hadi minne ili mimea hiyo ianze kuzaa matunda.

Mkulima huyo anasema kuwa, mmea mmoja wa mchenza hutoa kilo zaidi ya 50 za matunda kwa msimu mmoja.

“Mmoja (mchenza) hutoa katoni mbili – ambapo moja huwa na kilo 27,” asema, akiongeza kuwa katoni mbili za matunda hayo huwa na kilo 54 kwa jumla.

Hata hivyo, anasema kuwa, machungwa huwa ni makubwa na yana uzani wa juu, ikilinganishwa na machenza.

“Lakini machungwa ni tofauti, utapata ni mazito kiasi. Machungwa katoni moja utapata ni karibu kilo 30 ama kilo 40. Mti mmoja unaweza kutoa maboksi matatu au manne,” aeleza mkulima huyo.

Mbithe anasema kuwa kuna changamoto kadha wa kadha ambazo wamezipitia katika ukuzaji wa mimea hiyo ya matunda, mathalani magonjwa na wadudu waharibifu wanaovamia mimea na matunda.

Benson Mbithe akiwa katika shamba lao la michungwa na michenza, katika kitongoji cha Katulyani, Kibwezi West, Kaunti ya Makueni. Picha | Peter Changtoek

“Kuna msimu ulio na mazao mengi na mwingine unapata machache,” asema, akiongeza kuwa, kuna dawa ambazo wao huzitumia ili kukabili changamoto ya magonjwa na wadudu.

Mbithe anasema kwamba, wao huzuia magonjwa kwa kunyunyizia dawa pindi tu dalili zinapoanza kuonekana.

Mbali na magonjwa na wadudu waharibifu wanaoivamia mimea na matunda, changamoto nyingine ambayo anasema kuwa wanapitia ni kiangazi ambacho huliathiri eneo hilo mara kwa mara.

Aidha, anadokeza kwamba kama mkulima hana hela za kutosha za kununua mafuta ya kutumia kwa jenereta ya kusukuma maji kutoka mtoni hadi shambani, mazao yatakayozalishwa yatakuwa machache na ya kiwango cha chini.

Mkulima huyo anafichua kuwa, wateja huenda kuyanunua matunda yao shambani. Wateja huuziwa machungwa kwa Sh30 kwa kilo moja. Hata hivyo, machenza huuzwa kwa bei ya juu ya Sh150 kwa kilo.

  • Tags

You can share this post!

Bingwa Eliud Kipchoge asubiriwa na kibarua kigumu katika...

Harambee Starlets waelekea nchini Cameroon kumenyana na...

T L