• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:55 AM
Kuhifadhi kumbukumbu za mitambo kuna manufaa tele

Kuhifadhi kumbukumbu za mitambo kuna manufaa tele

Na RICHARD MAOSI

MITAMBO ya kuendeleza kilimo-biashara inahitaji matunzo ya hali ya juu, ili kumpatia mkulima natija ya muda mrefu, kwenye shughuli za kuendesha kilimo endelevu.

Apatie kipaumbele gharama ya kuajiri kibarua mwenye ujuzi wa kutosha, ikizingatiwa kuwa sio wakulima wengi mashinani wana uwezo wa kutumia mitambo ya kisasa hususan ile inayoendeshwa na kawi ya mvuke au upepo.

Lakini inapokuja katika utumiaji wa masine zinazohitaji nguvu za binadamu (manual machines), sio lazima kusaka huduma za mtaalam kwani aghalabu huwa ni nyepesi kuendesha na zinahitaji kuwekewa kumbukumbu

“Ni kwa sababu hiyo mtumiaji atakuwa katika nafasi nzuri ya kukarabati mitambo yake inapoanza kuonyesha dalili za kuchakaa, ikiwa ni baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu,” anasema Charles Ouma kutoka eneo la Ahero kaunti ya Kisumu.

Ouma ni mwenyekiti wa chama cha ushirika ambacho kinawaleta pamoja zaidi ya wakulima 80 ambao wanaendesha shughuli mbalimbali za kilimo pamoja na kuongezea matunda thamani.

Anasema kuwa usindikaji ni shughuli ambayo haiwezi kufanikiwa bila wakulima kuwekeza ipasavyo kwa mitambo ya kisasa.

Kwa wiki moja ni kundi ambalo linaweza kutengeneza zaidi ya kilo 500 ya unga wa mihogo , akielezea kuwa mafanikio yao makubwa yanatokana na ujuzi wa kutumia mitambo, na upatikanaji wa soko la uhakika.

Katika hatua ya kwanza amebaini kuwa kilimo cha kutumia masine za kisasa kina uwezo mkubwa wa kuwavutia vijana shambani.

Hii ni kwa sababu kumbukumbu zinaonyesha kuwa vijana wengi wanaotembelea viwanda au makundi ya kufanya usindikaji, huwa wanatafuta kazi kwenye vitengo vya kutumia mashine, karne hii ya teknohama.

Kwa kuwa hii ni mitambo inayotumia mikono, anaamini kuwa ni jambo la kimsingi kwa mkulima kuweka kumbukumbu za matumizi na maelezo mafupi kuhusu mitambo.

Bila kusahau kuwa kuongeza viwango vya kutumia masine kunaimarisha mchakato wa kijamii na kiuchumi kwa shughuli za shambani.

Isitoshe anaongezea kuwa mkulima ahifadhi historia ya awali ya mitambo yake, ikiwemo ni pamoja na gharama ya kukarabati ili iweze kubainika endapo anatengeneza faida ama hasara.

Kulingana naye utafiti unaonyesha kuwa masine ambayo haijakaguliwa vilivyo kabla na baada ya kutumika huwa katika uwezano mkubwa wa kushindwa kufanya kazi, labda inaweza kushika kutu au kukwama kazini.

Hata hivyo anaelezea kuwa usindikaji ni shughuli muhimu ambayo haiwezi kufanyika bila ya mitambo , kuna masine za kuvuna, kupakia , kusafisha na kuhifadhi mboga au matunda.

Kulingana naye anasema kuwa mkulima anafaa kuhifadhi vyombo vyake katika mazingira ambayo ni safi na salama, mbali na wanyama au watoto.

Kuvalia mavazi mwafaka wakati wa kutumia masine za shambani ni jambo la kimsingi, hii ni hatua ambayo hupunguza visa vya uwezekano wa ajali kutokea, kwa mfano mtumiaji anashauriwa kuvalia magwanda maalum ya kichwa, glavu na kuhakikisha ana nywele fupi.

Aidha anasema kuwa mkulima ambaye anaelewa mitambo yake vyema anaweza kuiangazia pale inapopata hitilafu ama kuharibika, hii ikitokana na juhudi zake kuhifadhi historia.

Aliongezea kuwa swala la kudumisha usafi kwenye mitambo humweka mkulima katika nafasi nzuri ya kugundua endapo mitambo yake imeanza kuchakaa.

Pili kutumia mitambo ya shambani mara kwa mara ni jambo la maana, kwani mitambo ambayo huwekwa ndani na kupumzishwa kwa muda mrefu bila ya kutumika, hupoteza thamani.

Anasema kuwa katika sehemu zinazozunguka, ulainishaji (lubrication)unahitajika ili kurahisissha mchalkato wa usindikaji kwa kuyageuza mazo hadi yawe vipande vidogovidogo.

You can share this post!

Anapenda upishi, sasa ana kiwanda cha kupika pilipili

Wazee waonya vikali ‘wanaouza’ baraka

T L